Wakurugenzi watano MSD watumbuliwa

18May 2022
Romana Mallya
DODOMA
Nipashe
Wakurugenzi watano MSD watumbuliwa

WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu, amesema wizara yake imeanza kuyafanyia kazi maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu Bohari ya Dawa (MSD) na kwamba wakurugenzi watano wa hapo wanawaondoa.

WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu.

Aliyasema hayo juzi jioni bungeni alipokuwa anahitimisha hoja ya makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2022/23 ambayo ilipitishwa na wabunge wote kwa kura ya ndiyo.

Alisema wakurugenzi wanaoondoka ni Mkurugenzi wa Fedha, Mkurugenzi wa Manunuzi, Mkurugenzi wa Vifaa, Mkurugenzi wa Sheria na Mkurugenzi wa Utawala.

Alisema ameshaielekeza MSD kwamba watawapima kwa upatikanaji wa dawa za miezi minne na siyo mwezi mmoja.

Waziri Ummy alisema wamewaeleza kuwa wanataka dawa zote 290 pamoja na vifaa tiba vipatikane.

"Katika hili tunamshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa maagizo yake tumeshaanza kuyafanyia kazi sambamba na Mheshimiwa Rais kubadilisha uongozi, Mtendaji Mkuu MSD pamoja na kumteua Mwenyekiti wa Bodi, tunawaondoa wakurugenzi watano wa MSD.

Waziri Ummy alisema

wameshauriwa pia kuangalia mifumo ya usambazaji wa dawa ndani ya MSD na kwamba wataendelea kuitaka inunue dawa na vifaa tiba kutoka viwandani kwa kuzingatia mikataba ya muda mrefu.

"Ninaomba niseme jambo moja, nimepewa dhamana ya kusimamia sekta ya afya hatutakuwa na upendeleo wa ubora wa dawa na vifaa tiba kwa sababu tusiende kuwapa matatizo Watanzania kwa kutoangalia ubora," alisema.

Waziri huyo alimpa pole Mkurugenzi mpya wa MSD ambaye amepewa hongera kwa kumweleza kuwa ana kazi kubwa kwa sababu matumaini ya Rais na wabunge pamoja na yeye ni makubwa.

"Mheshimiwa Spika, tuseme (Mkurugenzi Mkuu) alikuwa ndiye mshauri wa serikali kuhusu masuala mazima ya dawa akiwa upande wa Ubalozi wa Marekani, Mwenyekiti wa bodi alikuwa mashauri wa serikali kwa upande wa Global Fund ambao ndiyo wanatupa dawa za Ukimwi, Kifua Kikuu (TB) na malaria.

"Juzi nilikuwa ninamwambia Mheshimiwa Waziri Mkuu ni sawa nyie si mnatukosoa, mnashauri haya sasa nendeni mkafanye hayo ambayo mlikuwa mnaeleza."

Waziri Ummy alisema Mkurugenzi Mkuu MSD wamemwambia ndani ya miezi mitatu dawa zifike katika vituo na hospitali.

Kuhusu matumizi ya dawa katika ngazi ya hospitali alisema MSD inaweza kuzipeleka lakini anahoji madaktari na wataalamu waliopo huko wanazingatia miongozo ya matibabu ya taifa.

"Kwa sababu zipo taarifa tumezipata dawa ambazo zipo katika hospitali zilizoagizwa na mfamasia, daktari anaandika za kwake mwenyewe ambazo ni kinyume, hili tutalisimamia kwa kiasi kikubwa," alisema.

Aliwataka wabunge wasaidie jambo hilo wanapokaa kwenye mabaraza ya madiwani wahoji kamati za afya za kusimamia vituo kama zinafanya kazi na kufuatiliwa upatikanaji wa dawa.

Waziri huyo alisema mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) itawasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha mnyororo mzima wa dawa.

Pia alisema kamati imetoa maoni kuhusu matumizi holela ya dawa ambayo ameahidi wataendelea kuyafanyia kazi.

Kadhalika alitaja eneo la mwisho katika dawa kuwa watafufua na kuimarisha uzalishaji wa dawa kwa kuvifufua viwanda ambavyo vilikufa.

BIMA YA AFYA

Waziri Ummy alisema wataendelea kutoa elimu kuhamasisha umuhimu wa kuwa na bima ya afya ili wapate matibabu.

"Tutakamilisha haraka muswada wa sheria. Kwa upande wa huduma za kinga Mheshimiwa (Erick) Shigongo amesema vizuri pamoja na Dk. Pauline Nahato na Cecilia Pareso ni kweli ukiangalia hii bajeti imezungumzia tu tiba tunatakiwa kujieleza kwenye kuzuia, ndiyo maana ukiniuliza nichague kipaumbele changu cha kwanza sina fedha nitafanya chanjo za watoto hii ni moja ya kuwakinga.

Habari Kubwa