Walemavu waguswa kuwekwa serikalini

03Dec 2018
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Walemavu waguswa kuwekwa serikalini

SHIRIKA la kimataifa la kuwasaidia watu wenye ulemavu wa ngozi la Under the Same Sun, limeipongeza serikali ya awamu ya tano kutokana na kuendelea kuwapa nafasi za juu za uongozi watu wenye ulemavu.

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Idara ya Ushauri wa Wanafunzi katika masuala ya ajira wa shirika hilo, Josephat Igembe, wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wanafunzi wenye ualbino waliohitimu katika vyuo mbalimbali nchini.

Alisema serikali ya awamu ya tano imetambua kwa kiwango kikubwa uwezo wa watu wenye ulemavu katika uongozi na kwamba kitendo hicho cha kuwapa nafasi kumesaidia kuonyesha uwezo wao na kubadilisha taswira iliyokuwapo katika jamii.

“Kwa kweli tukilalamika tena kwamba hatujapewa nafasi tutakuwa tumekosa fadhila kwa serikali na kwa Mungu pia, tunazungumza bila kumung`unya maneno, awamu hii imetambua uwezo wa watu wenye ulemavu na imetupa nafasi,” alisema Ugembe na kuongeza:

“Na hatua hiyo ya serikali kuwapa wenye ulemavu nafasi kuonyesha uwezo wao, imeanza kuleta mabadiliko katika jamii, ile kasumba iliyokuwa imejengeka kwamba hawawezi, sasa imeanza kuleta mabadiliko taratibu na tunaamini hali hii ikiendelea hali hiyo itaisha kabisa.”

Pia Igembe alisema pamoja na serikali kutoa nafasi hiyo kwa kundi hilo, lakini changamoto imebaki kwa sekta binafsi ambao pamoja na sheria ya ajira kutaka kuajiri asilimia tatu kutoka katika kundi hilo, lakini wengi wamekuwa hawazingatii.

Kwa upande wake Mhitimu wa Chuo Kikuu cha Utumishi wa Umma katika Shahada ya Usimamizi wa Fedha katika sekta ya umma, Denis Otaru, alisema vijana wengi wa kitanzania bila kujali wana ulemavu ama laa wanashindwa namna ya kujiuza katika ushindani uliopo kwenye sekta ya ajira, jambo linalosababisha wengi wao kukosa kazi ingawa wamefaulu vizuri.

 

 

 

Habari Kubwa