Walengwa uboreshaji wa Daftari Mpigakura

24Jun 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Walengwa uboreshaji wa Daftari Mpigakura

UBORESHAJI wa Daftari la Kudumu la Mpigakura linalotarajia kuanza mwezi ujao, litahusu kurekebisha taarifa za wapigakura, kuhamisha taarifa za waliohama, kuwaondoa waliopoteza sifa na kutoa kadi mpya kwa waliozipoteza na zilizoharibika.

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dk. Athuman Kihamia.

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dk. Athuman Kihamia, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa semina waliyoitoa kwa wahariri na waandishi wa habari.

Akizungumza kuhusu uboreshaji wa daftari hilo, Dk. Kihamia alisema uboreshaji utahusu raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 18 na zaidi na wale ambao watakuwa wametimiza umri wa miaka 18 siku ya uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika mwakani.

“Kumefanyika uhakiki wa vituo vya kuandikisha wapigakura baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Uhakiki huo ulilenga kuweka vituo katika maeneo yaliyokubalika pamoja na kuweka angalau kituo kimoja katika kila mtaa au kijiji kwa kuzingatia umbali na idadi ya watu eneo husika,” alisema.

Alisema maeneo yaliyokubalika kwa mujibu wa Kanuni ya 12(2) ya Kanuni za Uboreshaji wa Daftari nchini ya Sheria ya Uchaguzi, sura ya 343 na Kanuni ya 15(2) ya Kanuni za Uboreshaji wa Daftari chini ya Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa sura ya 292 ni majengo ya umma na yale ya wazi yanayofikika kwa urahisi.

Maeneo yasiyokubalika kuwa ni kambi za jeshi, nyumba za ibada, ofisi za vyama vya siasa, kambi na makazi ya polisi.

Dk. Kihamia alisema mpigakura ambaye hatakuwa na kadi yake ya awali, taarifa zake zitatafutwa ndani ya mfumo.

“Endapo taarifa zake hazitapatikana, mpigakura ataandikishwa upya kwa kujaza fomu namba moja na uchukuaji alama za vidole, picha na saini litaendelea na atapatiwa kadi mpya,” alisema.

Kuhusu wale waliopoteza kadi au wale zilizoharibika, Dk. Kihamia alisema watajaza fomu namba 5A na kuipeleka kwa BVR (kit operator) ili kupatiwa kadi mpya.

“Katika uboreshaji wa daftari, wapigakura ambao watakuwa wamepoteza sifa za kuendelea kuwapo kwenye daftari mfano waliofariki, wanatakiwa kuondolewa, watu wenye taarifa kuhusu watu hao wanatakiwa kuzipeleka katika vituo vya uandikishaji kipindi cha uboreshaji na kujaza fomu namba 5B,” alisema.

Alisema Ofisa Mwandikishaji ataziwasilisha fomu hizo tume kwa sababu ndiyo yenye jukumu la kuwaondoa watu hao waliopoteza sifa.

Alisema baada ya uboreshaji kukamilika, NEC itaandaa Daftari la Wapigakura ambalo litatumika katika uchaguzi.

“Tume itakuwa na utaratibu wa kutoa nakala ya Daftari la Wapigakura kwa vyama vya siasa kabla ya uchaguzi mkuu, baada ya kukamilisha kila chama cha siasa kitapewa nakala yake,” alisema.

Habari Kubwa