Walia na polisi kifo cha ndugu yao

19Mar 2017
Robert Temaliwa
Nipashe Jumapili
Walia na polisi kifo cha ndugu yao

SIKU chache tangu mkazi wa Kijiji cha Kwampapayu, Muheza Mkoani hapa, Abubakar Mkangara (36) auawe kwa kukatwa katwa na mapanga na kundi la watu wasiojulikana, familia yake imeliomba Jeshi la Polisi kuwasaka waliohusika ili sheria ichukue mkondo wake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba.

Wakizungumza na Nipashe nyumbani kwa marehemu juzi, wanafamilia hao walisema tukio hilo limewaachia simanzi kubwa kutokana jinsi ndugu yao alivyouawa.

Kaka wa marehemu, Mohamed Mkangara, alisema siku ya tukio hilo wakati mdogo wake akitokea katika kijiji cha Mkuzi kwenda nyumbani kwake, alipofika katika shamba lake alikutana na kundi la watu likiwa na mapanga na mbwa na kuanza kumfukuza kama mhalifu.

Mkangara alisema ndugu yake alipoona kundi hilo la watu linamfukuza na mbwa, alikimbia huku akipiga kelele za kuomba msaada lakini hakufanikiwa kupata msaada wowote.

Alisema baadaye aliishiwa nguvu ndipo kundi hilo lilipomkamata na kuanza kumcharanga mapanga katika sehemu mbalimbali za mwili kisha kumwacha akiwa anatokwa na damu kwa wingi.

Aliongeza kuwa baada ya kundi hilo kumwacha akiwa hoi, wasamaria wema waliomwona akifanyiwa unyama huo walitoa taarifa polisi hatimaye kufika na kumpeleka katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Muheza, lakini alifia njiani kutokana na kutokwa damu nyingi.

Naye baba mdogo wa marehemu, Mganga Mkangara, alisema licha ya mwanawe kufanyiwa unyama huo, hakuwa na ugomvi na mtu yeyote zaidi ya kwamba alikuwa akilalamika kuibiwa na kuharibiwa mazao yake shambani na watu wasiojulikana.

“Tunaliomba jeshi la polisi lifanye uchunguzi wa kina ili kuwabaini watu waliohusika na mauaji hayo ya kinyama ili sheria ichukue mkondo wake dhidi ya wahusika wote," alisema Mkangara.

Alisema licha ya kwamba ndugu yao ameshakufa, wanaomba haki itendeke kwa hatua kali kuchukuliwa kwa wahusika wote.

Habari Kubwa