Walilia uhaba taulo za kike

23Mar 2019
Steven William
Muheza
Nipashe
Walilia uhaba taulo za kike

WANAFUNZI wanaosoma katika shule za sekondari mkoa wa Tanga wamelalamikia kukosekana kwa taulo za kike, hivyo kufanya kuwa kero kwao katika kujisitiri wanapokuwa madarasani au katika shughuli zingine.

Hayo waliyasema juzi katika risala ya mtandao wa Tanga Fema Club Mentors, iliyosomwa na Mwanaisha Lissu mbele ya mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Muheza,  Mwanasha Tumbo,  kwenye tamasha lililofanyika katika Shule ya Msingi ya Magila.

Alisema watoto wa kike katika shule nyingi za sekondari mkoa wa Tanga wanakosa taulo za kike, hivyo kuwafanya wawe katika mazingira magumu wakati wa masomo na shughuli zingine.

Lissu alisema kuwa klabu za Fema zina changamoto nyingi kama vile kukosa muda wa kutosha katika kufanya shughuli kwa ufanisi. Pia alisema zinakosa rasilimali fedha na mapokeo hasi kwa jamii kuhusu shughuli za mtandao huo.

Kuhusu mafanikio ya mtandao huo katika mkoa huo, alisema klabu zimekuwa zikishiriki kongamano la vijana kitaifa la Femina kila mwaka, mtandao wa mkoa wa Tanga umepata tunzo ya mkoa bora kitaifa mwaka 2019.

Mwenyekiti wa Fema Mkoa wa Tanga, Mayombo Charles, alisema mkoa wa Tanga una klabu 118 za Fema katika wilaya zote nane ambazo ziko katika mtandao wa malezi ya vijana ambao ulianzishwa mnamo mwaka 2017.

Wakati huo huo, wanafunzi wanaosoma shule mbalimbali za sekondari katika mkoa wa Tanga wameiomba serikali kutoa adhabu kali kwa wanaume wanaowapa mimba wanafunzi wa kike ili kukomesha mimba za utotoni.

Ibrahim Athumani, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Songa na Mwanahawa Mohamed wa Shule ya Sekondari ya Kerenge zote za Muheza na Kiondo Kilua wa Kwagunda wilayani Korogwe, kwa nyakati tofauti walisema wanaume wanaofanya hivyo wapewe adhabu kali.

Habari Kubwa