Walimu 800 wahitajika

14Feb 2018
Rahma Suleiman
Nipashe
Walimu 800 wahitajika

WALIMU wapatao 800 wanahitajika katika shule mbalimbali visiwani Zanzibar, ili kupunguza uhaba wa walimu nchini.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Zanzibar (ZATU), Mussa Omar Tafutrwa, katika mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika visiwani Zanzibar.

Alisema kuwa mfumo wao wa elimu unakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo  la upungufu wa walimu, vifaa vya kusomeshea na uhaba wa madarasa.

Alisema, kwa upande walimu kumekuwapo na upungufu mkubwa na kisiwani Pemba hali ni mbaya huku upande wa Unguja ni kwa baadhi ya mikoa ikiwamo Kaskazini na Kusini.

“Upungufu wa walimu upo kama tulivyosema kisiwani Pemba na kwa utafiti utulioufanya ndani ya chama chetu walimu wanaohitajika Pemba ni zaidi ya 800,” alisema.

Kuhusu upungufu wa vifaa vya kusomeshea alisema kuwa imetokea baada ya michango ya wanafunzi kwa wazazi kusitishwa na shule wakati mwengine zinakabiliwa na upungufu wa fedha za kujiendesha.

Waliomba kuwekewa fungu la fedha kwa ajili ya shule, ili kukidhi hali halisi ya upungufu huo wa fedha katika shule zao.

Akizungumzia upungufu wa madarasa, alisema unasababisha msongamano mkubwa wa wanafunzi na kufikia watoto 70 hadi 100 kukaa darasa moja ingawa hali hiyo imekuwa ikionekana kuwa ni ya kawaida.

Aliiomba jamii na serikali kuendelea na bidii ya kujenga vyumba vya madarasa ili yawe na hali bora zaidi. 

Habari Kubwa