Walimu kuandamana kupinga udhalilishaji

14Feb 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Walimu kuandamana kupinga udhalilishaji

KATIBU wa chama cha walimu wilayani Chamwino mkoani Dodoma (CWT) James Puya, amesema wanajipanga kufanya maandamano kushinikiza kigogo mmoja (jina tunalo) anayeshughulikia elimu wilayani humo kuchukuliwa hatua kwa madai ya kumpiga kibao mwalimu mwenzao mwandamizi wa Shule ya Msingi Ikombolinga.

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknoloji na Ufundi, Dk.Joyce Ndalichako

Akizungumza na NIPASHE ofisini kwake jana, katibu huyo alisema kuwa wapo katika hatua za kuomba kibali polisi ili wapate ruhusa ya kufanya maandamano hayo ambayo yatakuwa ya amani, lengo likiwa ni kuushinikiza uongozi kuchukua hatua dhidi ya mtumishi huyo ambaye mwandishi hakuweza kumpata ili kuzungumzia tuhuma hizo.

Puya alisema kuwa Januari 17 mwaka huu, kigogo huyo, alimpiga kibao mwalimu mmoja anayefundisha shule ya Ikombolinga wilayani hapa, kutokana na madai ya kuchelewa kwake kwa dakika 40 kuingia katika ukimbi uliokuwa wa semina kuhusu dhana ya Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).

Aidha, alisema kuwa kigogo huyo alimpiga kibao mwenzao na kumdhalilisha mbele ya walimu wengine, hali iliyosababisha CWT kulaani vikali tukio hilo na kuzitaka mamlaka husika kuchukua hatua stahiki kwa mtumishi huyo wa umma aliyekiuka maadili.

Alisema kuwa wameamua kufanya maandamano hayo ili kuusukuma uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kuchukua hatua kutokana na ukweli kuwa hadi sasa, hakuna kilichofanyika na mtuhumiwa anaendelea kufanya shughuli zake kama kawaida.

“Sisi (CWT) kama chama, tumeona kuwa bila kufanya maandamano haya, hakuna kitakachofanyika kwani viongozi wa halmashauri wapo kimya kana kwamba aliyepigwa kofi siyo binadamu,” alisema Puya.

Aliongeza kuwa kigogo huyo kuachwa bila kuchukuliwa hatua ni kikwazo kwa walimu ambao baadhi wamekuwa wakishindwa kufanya kazi zao kwa ufanisi kutokana na uwapo wake kwani licha ya tukio hilo la kumpiga kibao mwenzao mbele ya hadhara, amekuwa pia akitoa vitisho mbalimbali kwa walimu.

Alifafanua kuwa maandamano hayo ambayo wamepanga kuyahitimisha katika ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo, yanatarajiwa kufanyika ndani ya wiki hii, yakijumuisha walimu wote na wanachama wa CWT wa wilaya ya Chamwino.

Aidha, alisema chama cha walimu kitaendelea na hatua zingine za kumsaidia mwalimu huyo kutafuta haki yake ikiwa ni pamoja na kumshitaki mhusika katika tume mbalimbali za maadili ya utumishi wa umma.

Habari Kubwa