Walimu Rombo waanza kulipwa madeni yao

11Apr 2017
Godfrey Mushi
Rombo
Nipashe
Walimu Rombo waanza kulipwa madeni yao

SERIKALI imeanza kulipa zaidi ya Sh. milioni 50.9 za madeni ya walimu wilaya ya Rombo ambayo hayahusiani na mishahara.

Katibu wa Chama cha Walimu (CWT) Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, Emanuel Rajab, amesema fedha hizo zinazolipwa zinatokana na madai yao ya muda mrefu waliyoyawasilishwa katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Taarifa ya serikali kulipa madeni hayo ilitolewa jana na katibu huyo wakati wa hafla ya kuwaaga walimu saba waliostaafu wilayani Rombo.

“Fedha ambazo tayari zimeanza kugawanywa kwa walimu ni zaidi ya Sh. milioni 50.9 ambazo zilikuwa hazihusiani na madai ya mishahara. Kwa hatua hiyo tunaishukuru serikali kwa kulipa angalau kiwango kidogo kwa sababu walimu walishaanza kukata tamaa ya kuendelea kufundisha,” alisema Emanuel.

Kwa mujibu wa CWT Wilaya ya Rombo, hadi sasa madai ya stahiki za mishahara ambayo serikali inadaiwa na walimu wilayani hapa ni zaidi ya Sh. bilioni nne.

Hata hivyo, alisema mpaka sasa kuna walimu wilayani humo hawajalipwa mishahara yao ya miezi mitano hadi sita, hali ambayo inachangia kuzorotesha maendeleo ya elimu kutokana na baadhi yao kutokuwa na moyo wa kufundisha hadi walipwe.

Kuhusu upandishaji wa madaraja, alisema wilaya ya Rombo ina walimu 900 ambao hawajapandishwa madaraja kwa muda mrefu na kwamba wanaitaka idara husika kutekeleza majukumu yake ya kiutumishi ipasavyo ili kumaliza malalamiko ya walimu.

Akiwa mkoani Kilimanjaro hivi karibuni, Naibu Katibu Mkuu wa CWT Taifa, Ezekiel Oluochi, alikaririwa na Nipashe akisema madai ya stahiki za walimu nchi nzima hadi sasa ni zaidi ya Sh. trilioni 1.116.

Habari Kubwa