Walimu waliokopa wafuatwa darasani

18May 2022
Shaban Njia
KAHAMA
Nipashe
Walimu waliokopa wafuatwa darasani

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida taasisi za fedha zinazotoa mikopo zimedaiwa kuwanyang'anya kadi za benki walimu walioshindwa kulipa madeni na wakati mwingine kufuatwa madarasani kudaiwa  katika Manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga.

Mwenyekiti wa Chama cha Walimu (CWT) katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Meshack Mashigala.

Baadhi ya taasisi hizo zimekuwa zikiwafuata walimu katika sehemu zao za kazi kuwadai madeni mbele ya wanafunzi bila kufuata au kuheshimu mikataba waliyoingia wakati wanakopeshana.

Hatua hiyo imetajwa kuwa sehemu ya vikwazo vinavyorudisha nyuma maendeleo ya elimu katika manispaa hiyo kwa kuwa walimu wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu wakihofia kuvunjiwa heshima mbele ya wanafunzi wao, kufungiwa ndani na kupokwa kadi zao za benki.

Mwenyekiti wa Chama cha Walimu (CWT) katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Meshack Mashigala alibainisha hayo juzi mkoani Shinyanga.

Alisema kila mwaka kumekuwa na matukio ya baadhi ya walimu kukamatwa na wakopeshaji wa mikopo aliyoiita 'umiza' na kufungiwa ndani katika ofisi zao wanaposhindwa kulipa mikopo kwa wakati, akisisitiza kuwa jambo hilo lisipotatuliwa wanafunzi wataendelea kukosa masomo na kushindwa kumaliza mihula.

“Walimu wangu wanapokopa tu riba inakuwa asilimia 20, wanakabidhi kadi za benki na kutoa namba za siri za benki  wakati wa marejesho wanakuta riba imepanda hadi asilimia 100, hali ambayo hawezi kulipa na anaanza kuishi kama ndege na shuleni anashindwa kuhudhuria vipindi alivyopangiwa kufundisha,”  alisema Mashigala

Aliwataka wakopeshaji wa mikopo hiyo kuacha kujichukulia sheria mkononi kwa kuwakamata na kuwafungia katika ofisi za walimu badala yake wakawafungulie mashtaka kisheria na siyo kuwadhalilisha mbele ya wanafunzi na jamii inayowazunguka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, George Kyando, alithibitisha kutokea kwa matukio hayo na kubainisha kuwa walimu hao wamekuwa wakifika polisi kuomba barua ili waende benki kuomba kadi nyingine kwa madai kadi ya mwanzo imepotea.

Alisema kumekuwa na matukio mengi ya aina hiyo, hivyo kuwapo ishara ya udanganyifu, shida kuu ikibainika kuwa ni mbinu ya walimu kuzikwepa taasisi au watu waliowakopesha fedha kwa riba kubwa.

''Ukopeshaji wa mitaani siku zote unazaa shilingi kwa shilingi na wanapokopa hukabidhi kadi zao za benki na namba za siri na mwisho wa mwezi aliyemkopesha ndiye anakwenda benki kuchukua kiasi alichomkopesha, jambo ambalo ni kinyume cha sheria mtu kutumia akaunti ambayo siyo yake,'' alionya.

Kamanda Kyando aliwataka walimu wanapohitaji mikopo kwenda kukopa katika taasisi za kifedha zinazotambulika na serikali ambazo watakopa na kukuachiwa kiwango kinachotakiwa kisheria.

Kwa mujibu wa mwongozo wa utumishi, kiwango cha makato katika mshahara wa mtumishi hakipaswi kuwa chini ya theluthi ya mshahara wake wote.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Sophia Mjema, alisema walimu hao wanakosea kuingia katika mikopo hiyo huku wakijua inawaumiza.

Alisema kitu kibaya zaidi wanasamilisha kadi zao za benki pamoja na namba za siri na kumtaka Kamanda wa Polisi kuangalia namna ya kulitatua jambo hilo.

Habari Kubwa