Walimu washauriwa kutojali hali

05Mar 2016
Efracia Massawe
Nipashe
Walimu washauriwa kutojali hali

BAADA ya shule nyingi za serikali kuwa na mrundikano wa wanafunzi katika madarasa, walimu wameshauriwa kutafuta njia ya kuwasaidia kielimu wanafunzi hao ili watimize malengo yao.

Waziri wa Elimu, Prof.Joyce Ndalichako

Aidha, wanafunzi nao wametakiwa kutoridhika na kiwango wanachopata mashuleni, badala yake wajitume kutafuta elimu zaidi itakayokuwa mwanga wa mafanikio yao ya sasa na baadaye.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Shule ya Sekondari ya St. Disas iliyopo Chamanzi mkoani Dar es Salaam, Michael Owiti, wakati akizungumza changamoto za sera ya elimu bure juzi.

Owiti alisema kuna changamoto nyingi zinazochangia wanafunzi wengi wasifikie malengo yao na kutaja miongoni mwa hizo kuwa ni wazazi kushindwa kufuatilia mwenendo wa mwanafunzi darasani.

Alisema jambo hilo linachangia wanafunzi wengi kuridhika na kiwango cha elimu wanayopata na kubweteka wakiamini matokeo yoyote watakayoyapata mzazi atawajibika.

“Moja kati ya changamoto iliyopo kwa shule nyingi nchini ni wazazi kutokuwa na utamaduni wa kufuatilia mahudhurio ya watoto wao shuleni," alisema Owiti na kueleza zaidi:

"Kitendo cha kumuacha mwanafunzi chini ya mwalimu, hasa kwa majukumu mbalimbali ya msingi, wanawaandaa kisaikolojia kutokuwa na nidhamu pamoja na kupuuza masomo.”

Alisema asilimia 70 ya wanafunzi waliomaliza kidato cha nne katika shule hiyo mwaka jana, ambayo ni wanafunzi 68, walifanya vizuri na kati yao 42 wamebahatika kuendelea na kidato cha tano.

Mmoja wa wahitimu hao wa kidato cha nne katika shule hiyo, Hussein Bakar (19), alisema baadhi ya wanafunzi walifeli mitihani kutokana na changamoto mbalimbali ikiwamo ya kufuata makundi mabaya.

“Unaweza kukuta mwanafunzi anauelewa mkubwa darasani na ni miongoni mwa wanafunzi wanaotegemewa kufaulu kitaaluma, ila kutokana na ushawishi wa makundi anarubuniwa na kuharibika dakika za mwisho za mtihani,” alisema Bakar.

Mwanafunzi mwingine, Lisa Magombeka, alisema baadhi ya wanafunzi wa kike wamekuwa wakijiingiza katika mahusiano ya kimapenzi wakati wa masomo na kuchangia kufeli kwao.

Mmiliki wa shule hiyo, Dk. Didas Masaburi, aliunga mkono maamuzi ya serikali ya kutoa elimu bure na kusema kama fursa hiyo ikitumiwa vizuri watapatikana viongozi wazuri watakaosimamia rasilimali za nchi.

“Pamoja na hayo naishauri serikali isimamie sekta zote ili kuona matokeo chanya katika sekta hizo hususani sekta ya elimu na afya kwa sababu mwalimu hapimwi kwa kuhesabu kazi ngapi amefanya bali hupimwa kwa matokeo ya kazi alizofanya ambazo zimezaa matunda,” alisema Dk. Masaburi.

Wanafunzi wawili kati ya 68 waliopata daraja la kwanza walipewa motisha ya Sh. 100,000 kila mmoja huku wale waliopata daraja la nne wakipewa ofa ya kusoma bure Chuo cha Manunuzi na Ugavi cha IPS.

Habari Kubwa