Walimu watakaokimbia nyumba kushushwa vyeo

20Dec 2016
Na Mwandishi Wetu
MOROGORO
Nipashe
Walimu watakaokimbia nyumba kushushwa vyeo

SERIKALI wilayani Mvomero, mkoani Morogoro, imeagiza kushushwa vyeo kwa walimu wakuu wa shule za msingi, watakaobainika kuzikimbia nyumba zilizojengwa kwa ajili yao na kwenda kuishi maeneo mengine.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mohamed Utaly, wakati wa uzinduzi wa mradi wa Shiriki shuleni, unaotekelezwa na asasi isiyo ya kiserikali ya CDTFN, kwa ufadhili wa Shirika la Twaweza, ukilenga kutoa motisha kwa walimu watakaohudhuria vyema shuleni, kuingia darasani na kufundisha.

Alisema katika ziara zake wilayani Mvomero, alibaini uwapo wa baadhi ya walimu wakuu kuzikimbia nyumba zao, zinazojengwa shuleni, jambo linalofanya kukosekana ufuatiliaji wa wanafunzi kitaaluma.

Alimuagiza Ofisa elimu wa wilaya hiyo, kuwabaini na kuwachukulia hatua walimu hao na viongozi wengine wakiwamo madiwani, maofisa watendaji kata,vijiji, na wenyeviti wa vijiji kuwafichua walimu hao.

Aidha, aliwataka viongozi hao kujitathmini na kujiuliza walipokosea, hadi wilaya hiyo kuzidi kufanya vibaya katika matokeo ya darasa la saba, kutoka nafasi ya pili na tatu, mwaka jana na miaka mingine nyuma, hadi kuwa nafasi ya sita.

Akizungumzia mradi huo uliozinduliwa na Mkuu huyo wa wilaya, kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Injinia Dk. John Ndunguru, Mkurugenzi wa asasi ya CDTFN, Felister Kalomo, alisema mradi huo umechaguliwa kutekelezwa katika wilaya mbili nchini, ikiwamo moja ya mjini na moja ya vijijini.

Habari Kubwa