Walimu watishia kupiga kambi ofisi za wabunge

06Mar 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Walimu watishia kupiga kambi ofisi za wabunge

CHAMA cha Walimu (CWT), Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, kimetishia kufanya maandamano kwenda kuweka kambi kwenye ofisi za wabunge watatu wa wilaya hiyo kama njia ya kuwashinikiza watatue kero zao.

Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa chama hicho wilayani Ilala, Emmanuel Kihako, wakati akizungumza na Nipashe kuhusu kero mbalimbali za walimu katika wilaya yake.

Kihako alisema hivi karibuni wanatarajia kwenda kwenye ofisi za Mbunge wa Ilala, Musa Azzan (CCM), Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) na Mbunge wa Segerea (CCM), Bonah Kaluwa, ili kuwataka wawasilishe bungeni madai ya walimu yanayoongezeka mwaka hadi mwaka.

“Hawa wabunge wetu ndiyo watu sahihi kutusemea shida zetu, lakini ni muda mrefu hatujawahi kuwasikia wakizungumzia shida zetu, walimu wana madai mengi sana serikalini, walimu hawapandi madaraja, hawajapata nyongeza ya mishahara, wanadai, waliokopa wanakatwa makato makubwa na Bodi ya Mikopo,” alisema Kihako.

Alisema nyongeza ya mishahara ambayo hutolewa kila Julai mosi, haikutolewa mwaka jana, hali ambayo alisema imewachanganya walimu na kwamba kwa kufanya hivyo mwajiri wao amevunja mkataba aliousaini mwenyewe.

“Sisi CWT Ilala, tunaiomba serikali itoe nyongeza ya mwaka 2016 kwani ni haki yetu kwa mujibu wa mkataba wetu, uhakiki gani unachukua mwaka mzima, mambo yamekwama ukiuliza wanasingizia uhakiki, CWT tuna manung’uniko makubwa, tunaomba watulipe,” alisema.

“Mwajiri alitoa taarifa kwamba ndani ya miezi miwili atakuwa anakamilisha zoezi la uhakiki wa wafanyakazi hewa na baada ya hapo taratibu nyingine zitaendelea. Lakini cha kushangaza hadi leo hii ni zaidi ya miezi sita hakuna kinachoendelea,” alisema Kihako.

Alimuomba Waziri wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Angella Kairuki, ashughulikie mkwamo huo haraka ili kuleta uhusiano mzuri kati ya watumishi na mwajiri.

Aidha, alisema Bodi ya Mikopo imekuwa ni kero kwa watumishi waliokopa kwa kuwakata marejesho ya asilimia 15 badala ya asilimia nane kama walivyokuwa wamekubaliana awali.

“Tunamwomba mwajiri kupitia Bodi ya Mikopo azingatie makubaliano ya kurejesha asilimia nane badala ya 15, kama sheria imerekebishwa kufikia makato ya asilimia 15, basi isiwaathiri waliokopeshwa kabla ya sheria hiyo mpya, kwa sasa kuna walimu wanakatwa fedha zote pasipokuzingatia kanuni,” alisisitiza Kihako.

Alitaja madeni ya walimu kwa mwaka 2015/2017 kwa elimu ya msingi kuwa likizo ni Sh. 709,688,300, matibabu Sh. 23,605,000, masomo Sh. 4,137,600, uhamisho 11,420,200, mazishi 2,280,000 na mizigo kwa wastaafu Sh. 299,643,600 ambazo zinafikia jumla ya Sh. bilioni 1.05.

Kihako alifafanua kuwa madeni wanayodai kwa upande wa elimu sekondari masomo ni Sh. 3,030,000, mizigo kwa wastaafu Sh. 57,379,200, likizo Sh. 67, 692, 000, matibabu 7, 923,000, uhamisho 13,678,000, kujikimu 2,258,000, likizo za Juni, 2016 ni Sh. 100,484,000 ambazo jumla yake zinafikia Sh. 252,444,200.

“Deni lote msingi na sekondari linafikia Sh. bilioni 1.3, hivyo tunamwomba Waziri Kairuki amshauri vyema Mheshimiwa Rais ili atatue changamoto hizi za walimu mapema ili kutowakatisha tamaa," alisema.

Habari Kubwa