Walimu wote kuhamishwa kisa vifo wanafunzi

30Jul 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Walimu wote kuhamishwa kisa vifo wanafunzi

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, ameagizwa kuwaondoa walimu wote wa Shule ya Msingi Mbori, wilayani Mpwapwa ili kupisha uchunguzi wa vifo vya wanafunzi watatu waliofukiwa na kifusi.

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka. picha mtandao

Waziri Ummy alisema watapelekwa walimu wengine na kwamba leo wanafunzi wataendelea na masomo.

Aidha, siku saba zimetolewa kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuchunguza vifo hivyo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu, alitoa kauli hiyo juzi aliposhiriki kuaga miili ya wanafunzi hao.

Akizungumza na wananchi, Waziri Ummy alilaani vikali vitendo vya walimu kuwafanyisha kazi zisizo stahili wanafunzi tofauti na ilivyoelekezwa kwenye waraka wa elimu bila malipo namba tatu wa mwaka 2016.

“Hatukatazi mwanafunzi kufanya kazi zinazomjenga kama vile stadi za kazi, lakini sio kumfanya mwanafunzi kama kibarua unawezaje kumwambia mtoto akachimbe mchanga wa kujengea au akaponde kokoto tena bila uangalizi wa walimu?”Alihoji.

Alisema katika shule hiyo kiasi cha Sh. milioni 12 kwa ajili ya ujenzi wa choo na fedha za mchanga zimejumlishwa humo na kuhoji sababu za walimu kuwatuma watoto kwenda kuchimba mchanga wa mtoni.

“Kuna uzembe hapa umefanyika na tutachukua hatua,” alisisitiza.

Aliwataka wakuu wa shule zote nchini na walimu wa ujumla kuacha kuwatumikisha wanafunzi wawapo shuleni na wazingatie waraka wa elimu bila malipo namba tatu wa mwaka 2016 ambao unatoa ufafanuzi wa kina wa jukumu la kila mdau wa elimu.

“Jukumu la ujenzi wa miundombinu ya shule ni la wazazi pamoja na jamii inayozunguka na sio wanafunzi, walimu na kamati za shule mnatakiwa kuhamaisha wazazi na jamii kujitolea kujenga miundombinu hiyo na sio kutumikisha wanafunzi,” alisisitiza.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Josephat Maganga, alisema watoto waliofariki kwenye ajali ya kufukiwa na kifusi shuleni hapo ni watatu ambao ni Isaya Lucas Hamis, Rehema Alex na Daud Enock Mchea na watoto wengine watano walijeruhiwa ambapo walitibiwa na kuruhusiwa kurejea majumbani kwao.

Julai 27, mwaka huu, watoto hao walifukiwa na kifusi baada ya kupewa kazi ya kuchimba mchanga na walimu wao kuchimba mchanga kwa ajili ya ujenzi wa choo unaoendelea shuleni hapo.