Waliohusika upotevu wa mapato ya umma kukiona

03Mar 2016
Mary Geofrey
Dar
Nipashe
Waliohusika upotevu wa mapato ya umma kukiona

NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo, amesema kuwa wizara yake itahakikisha inawachukulia hatua kali za kisheria na kinidhamu watumishi wa halmashauri nchini.

Naibu Waziri, TAMISEMI, Seleman Jafo.

Watumishi hao ni waliowahi kuhusika na upotevu wa mapato ya serikali hata kama walishaondolewa kazini.

Jafo aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na wakuu wa idara na vitengo wa Halmashauri ya Kinondoni.

Aliwaagiza wahakikishe wanasimamia vyema majukumu yao hasa kuwatekelezea mahitaji na madai ya watumishi walioko chini yao wakiwamo walimu na wauguzi.

Pia aliwataka waache malumbano wakati wa utekelezaji wa majukumu ya kazi na badala yake kila mtumishi asimamie vyema sekta yake ili kuiendeleza.

“Halmashauri hii inaongoza kwa kukusanya mapato, lakini kuna watumishi wachache wanakwamisha kazi zinazofanywa na halmashaiuri hii. Sasa nawahakikishia Tamisemi haitawaacha, lazima watachukuliwa hatua hata kama walishaondoka kazini na ni halmashauri zote nchini,” alisisitiza Jafo.

Sambamba na hilo, pia aliiagiza halmashauri hiyo kuhakikisha inaharakisha kupata eneo la ujenzi wa machinjio ya kisasa kwani zilizopo haziendani na hadhi ya halmashauri hiyo.

“Nimkwenda machinjio ya Kimara Stop Over, mazingira yake ni aibu, lakini pia idadi ya ng’ombe ambao wanaotambulika wanachinjwa pale ni 100 hadi 120, ila kiuhalisia ng’ombe zaidi ya 300 wanachinjwa pale kila siku, ushuru wa ng’ombe hao haujulikani unakokwenda. Inawezekana mwenye machinjio yale yuko hapa halmashauri na ndiyo maana hatua hazichukuliwi,” alisema Jafo.

Vile vile aliwataka kuongeza kiwango cha ukusanyaji wa mapato yatokanayo na majengo kama walivyejiwekea ambapo mwaka huu wamelenga kukusanya Sh. bilioni tisa.

Kwa upande Meya wa manispaa hiyo, Boniface Jacob na Naibu Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Ando Mwankuga, walimuahidi Jafo kuwa watatekeleza yote aliyoyaagiza na kumhakikishia kuwa halmashauri hiyo itaendelea kuongoza.

Habari Kubwa