Walioigiza maiti wagoma kuwekwa mochwari

15Mar 2016
Lulu George
Nipashe
Walioigiza maiti wagoma kuwekwa mochwari

ABIRIA watano wa ajali ya ndege waliokuwa wakishiriki katika uokoaji kwenye kiwanja cha ndege cha Tanga, wamezua taharuki kwa watumishi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Tanga ya Bombo, baada ya kugoma kuhifadhiwa kwenye majokofu ya chumba cha maiti.

MAJENGO YA HOSPITALI YA BOMBO

Abiria hao, ambao walifikishwa kwenye chumba hicho saa 5.30 asubuhi, wakidhaniwa ni marehemu, walipokelewa kama maiti na ghafla wakati wakitaka kuingizwa kwenye majokofu, waliposhuka kwenye machela na kugoma kuingia wakisema hapo ndiyo mwisho wa mchakato wao wa uigizaji.

Jana, saa 5:00 asubuhi, Jiji la Tanga lilishtushwa na askari wa usalama barabarani wakizuia magari ya watu binafsi ili kupisha magari ya uokoaji yakiwamo ya zimamoto, ya kubebea wagonjwa kutoka hospitali mbalimbali za serikali na binafsi, huku kukiwa na taarifa kwamba kuna ndege ya abiria kutoka Pemba kwenda Tanga, imeanguka na kusababisha vifo vya abiria watano na wengine 12 kujeruhiwa.

Taarifa hizo zilisababisha viongozi wa taasisi zote zilizopo mkoani hapa kukimbilia eneo la uwanja wa ndege, akiwamo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Leonard Paulo, pamoja na viongozi wa vikosi vya ulinzi na usalama.

Katika kiwanja hicho, pia walikuwako watu ambao walidai kulikuwa na ndugu zao waliokuwa wamepanda ndege hiyo.
Nipashe ilifika eneo la tukio na kukuta waandishi wa habari wakiwa wamewekwa kwenye chumba maalumu kwa madai kwamba wametakiwa wakae nje ya eneo la tukio, kutokana na sababu za kiusalama.

Hata hivyo, saa 7.00 mchana alitoka Kamanda Paulo. Waandishi wa habari walipotaka kumhoji, alisema yeye si msemaji wa tukio hilo bali mwenye dhamana ni Meneja wa Kiwanja cha ndege cha Tanga.

Meneja wa kiwanja hicho, Mariam Ngowi, alisema zoezi hilo ni la kawaida kufanyika katika viwanja vya ndege, kupima taasisi mbalimbali zinavyojipanga katika kukabiliana na majanga.

“Tunashukuru kwa mwitikio wenu. Kweli mmeonyesha kwamba mko kazini muda wote kwani zoezi letu limeenda vizuri. Tulitengeneza vifo vitano na majeruhi 19 ambao walipokelewa katika hospitali za Bombo, Ngamiani na Tumaini,” alisema Ngowi.

Alisema hali halisi imeonesha kuwa watendaji wa taasisi za serikali na binafsi zinaweza kukabiliana na majanga ya kushtukiza bila kuwepo kwa vikwazo na ushirikiano wa hali ya juu.

Habari Kubwa