Waliojificha mapango ya Amboni ni wahamiaji haramu, asema RC Shigela

20May 2016
Lulu George
Tanga
Nipashe
Waliojificha mapango ya Amboni ni wahamiaji haramu, asema RC Shigela

SERIKALI mkoani hapa imetoa ufafanuzi kuwa watu waliojificha kwenye mapango ya Amboni yaliyopo Jijini Tanga ni wahamiaji haramu ambao waliingia nchini kinyume cha sheria.

mapango ya Amboni.

Wahamiaji hao haramu ndiyo wanaodaiwa kuhusika na matukio mbalimbali ya uhalifu ikiwamo mauaji ya watu watano yaliyotokea katika duka la bidhaa za jumla la Central Bakery mwishoni mwa Aprili, mwaka huu.

Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Tanga, Martine Shigela, alisema wahamiaji hao haramu wametumia eneo hilo la mapango ya Amboni kama sehemu yao ya maficho na hutoka pale tu wanapokuwa na mahitaji ya chakula.

Shigela ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, alisema kuwa kutokana na hali hiyo wameunda kikosi kazi ambacho kimeanza kazi rasmi ya kupambana na watu hao ambapo wapo Jeshi la Polisi, Jeshi la Wananchi
wa Tanzania (JWTZ ) na Uhamiaji.

Alisema mkoa huo unakabiliwa na changamoto kubwa tatu za kihalifu ambazo kikosi kazi hicho kitapambana nazo ikiwamo dawa za kulevya, biashara za magendo na uvuvi haramu.

“Hakuna ugaidi kama inavyoelezwa hawa walioweka kambi ni wahamiaji haramu ambao wametumia Tanga kama njia ingawaje kimsingi hawajui wanakoelekea sasa wanaingia kwenye maduka kutokana na njaa na kufanya uhalifu maeneo makubwa wanayojificha ni maporini na mapangoni,” alisema Shigela.

Hata hivyo, alisema kuwa zipo oparesheni za doria zinazoendelea kufanyika kwenye maeneo ya bahari ya Hindi, mpaka wa Horohoro unaotenganisha Tanzania na Kenya pamoja barabara kuu ya Tanga hadi Kilimanjaro.

Kufuatia hatua hiyo alitoa tahadhari kwa wakazi wa mkoa huo kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa mara wanapowatilia shaka watu ambao ni wageni kwenye maeneo yao.

Sambamba na rai hiyo pia Mkuu huyo wa Mkoa aliwaagiza viongozi wa Serikali za Vijiji, Mitaa na Vitongoji kufanya mazoezi ya utambuzi wa wageni kwenye maeneo yao na kukusanya taarifa zao ikiwamo shughuli
wanazozifanya.

”Na hii si kwa viongozi peke yake bali kwa wamiliki wa hoteli na nyumba za kulala wageni wote watupatia taarifa za wageni wanaoingia kwenye maeneo yao kwa kweli tunahitaji ushirikiano wa hali na mali
katika kukabiliana na hali hii kwani inarudisha nyumba maendeleo ya mkoa wetu,” alisisitiza.

Kwa mujibu wa Shigela ni kwamba katika kipindi cha Januari hadi Aprili mwaka huu takribani wahamiaji haramu 134 waliongia nchini bila kibali walikamatwa na kwamba idadi hiyo ni sawa na asilimia 50 ukilinganisha na takwimu za mwaka jana.

Takwimu za mwaka jana 2015 katika kipindi kama hicho, ni wahamiaji haramu 84 waliokamatwa.

”Hali hii inaonyesha kuwa vyombo vya dola vimeweza kudhibiti ile mianya yote ambayo walikuwa wakiitumia kupita, lakini niseme kwamba hatupo tayari kuruhusu watu waendelee kuharibu amani yetu na kutishia
usalama tutawakamata na hatua za kisheria zitaendelea kuchukuliwa dhidi ya wahusika,” alisema.

Matukio ya uhalifu yaliyofanyika kwenye maeneo mbalimbali mkoani hapa yalizua taharuki kwa wananchi na kuwa na hofu juu ya usalama wa maisha yao.

Kutokana na hilo wafanyabiashara wamekuwa wakifunga maduka yao saa 12.00 jioni kwa hofu ya kuvamiwa na wahalifu.

Habari Kubwa