Waliokaidi wito wa TRA kupewa kibano

21Jan 2019
Salome Kitomari
DAR ES SALAAM
Nipashe
Waliokaidi wito wa TRA kupewa kibano

MAMLAKA ya Mapato (TRA), imesema kuwa ambao hawakuitikia wito wa kulipa kodi bila riba kwa kipindi cha siku 100 wataanza kuilipa kwa mujibu wa sheria.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo.

Akizungumza mwishoni mwa wiki na Nipashe, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema kwa sasa ambao hawakuitikia wito huo watatakiwa kulipa kodi inavyotakiwa.

“Kwa mujibu wa sheria kamishna amepewa mamlaka ya kusamehe chini ya asilimia 50, sasa kama wapo ambao hawakulipa kwa muda uliotolewa wajue kuanzia sasa kamishna ataangalia kama wanastahili kuondolewa riba au kulipa kwa ukamilifu,” alisema.

Alisema kwa sasa TRA inafanya tathmini kujua waliolipa na ambao hawajalipa na kufuatiwa na ufuatiliaji wa kina kuhakikisha malimbikizo yote ya kodi yanalipwa inavyotakiwa.

Julai mwaka jana, TRA ilitangaza vigezo sita kwa wanaostahili kupata msamaha wa riba na adhabu kwenye malimbikizo ya madeni ya nyuma ya kodi.

Tangazo hilo lililokuwa limesainiwa na Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere, lilibainisha kuwa uamuzi huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais John Magufuli dhidi ya malalamiko ya wafanyabiashara nchini.

Katika Mkutano wake na Baraza la Taifa la Wafanyabiashara (TNBC) Machi 20, mwaka jana, walilalamikia kuwapo kwa malimbikizo makubwa ya madeni ya kodi za nyuma yakijumuisha riba na adhabu.

Vigezo vilivyotajwa ni kuwa ni wafanyabiashara waliowasilisha ritani za kodi, lakini bado wanadaiwa kodi yote au sehemu ya kodi zitokanazo na ritani hizo.

 Wafanyabiashara ambao hawajawasilisha ritani za kodi na wana madeni ya kodi ambao walikuwa wanafanyabiashara bila kusajiliwa na kupatiwa namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN), namba ya usajili wa kodi ya ongezeko la thamani (VRN) (VAT Registration Number) au usajili mwingine wa kodi kwa mujibu wa sheria zinazosimamiwa na TRA.

Wengine ni waliowasilisha pingamizi za kodi kwa Kamishna Mkuu na ambao pingamizi zao zinashughulikiwa katika ofisi za TRA na siyo kwenye mahakama za kikodi.

Kwa mujibu wa Kichere, wafanyabiashara ambao wamewasilisha pingamizi katika mahakama za kikodi na mashauri yao bado hayajatolewa maamuzi; na ambao wana madeni ya nyuma ya kodi ambayo hayatokani na kesi za jinai za kodi, utakatishaji fedha, usafirishaji wa binadamu au shughuli nyingine haramu.

“Mlipakodi atastahili kupata msamaha wa riba na adhabu endapo yeye binafsi au mwakilishi wake aliyeidhinishwa kisheria atawasilisha maombi ya msamaha kwa kujaza fomu maalum,” alifafanua.

Wafanyabiashara hao walitakiwa kuambatanisha maelezo ya kuonyesha kiasi anachodaiwa pamoja na kukubali kwa hiari kulipa deni lake la msingi; kukubali kwa maandishi kulipa kiasi chote cha kodi bila riba na adhabu ndani ya mwaka wa fedha 2018/19 ikiwa na maana kabla au ifikapo Juni 30, mwaka huu.

Aidha, wafanyabiashara hao walitakiwa kukubali deni la kodi alilokadiriwa na kuwa tayari kutoendelea na pingamizi au shauri husika la kodi lililowasilishwa kwa Kamishna Mkuu, Bodi ya Rufani za Kodi au Mahakama ya Rufani.

Tangazo hilo lilibainisha kuwa msamaha wa riba na adhabu utahusu kodi zote zinazotozwa kwa mujibu wa sheria zinazosimamiwa na TRA isipokuwa ushuru wa forodha chini ya sheria ya ushuru kwa mujibu wa sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004.

Kadhalika, mapato mengine yasiyo ya kodi ambayo TRA imepewa jukumu la kisheria la kuyakusanya kama vile kodi za majengo na ada za matangazo.

Habari Kubwa