Waliokufa kwa kimeta waongezeka, 97 wahofiwa kuambukizwa

28Feb 2019
Na Waandishi Wetu
Moshi
Nipashe
Waliokufa kwa kimeta waongezeka, 97 wahofiwa kuambukizwa

WATU wengine wawili wamepoteza maisha kwa ugonjwa unaodaiwa kuwa kimeta, huku watu 97 wanaohofiwa kuambukizwa wakilazimika kupewa chanjo kukabiliana na maambukizi ya vimelea hatari.

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Anna Mghwira, picha mtandao

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Anna Mghwira, amesema mpaka sasa watu watano wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Misheni ya Kilema inayomilikiwa na Kanisa Katoliki na wengine watatu wamelazwa katika Hospitali ya Rufani ya KCMC.

Watu hao wanasadikiwa kula mzoga wa ng’ombe mwenye vimelea vya kimeta katika Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

"Watu hao watano wanapatiwa matibabu baada ya kula mzoga wa ng’ombe wenye ugonjwa wa kimeta katika Wilaya ya Moshi na tayari watu 97 wameshapatiwa chanjo ya ugonjwa huo katika wilaya tatu za Mkoa wa Kilimanjaro.

"Ugonjwa huo ni hatari na unaambukizwa kwa njia ya hewa na hata kushikana, hivyo waliopoteza maisha wote watazikwa chini ya uangalizi," alisema.

Kwa mujibu wa Dk. Mghwira, watu hao wamekutwa na umauti na wengine kujikuta hospitali kutokana na kula mzoga wa ng’ombe ambao haujapimwa na wataalamu.

Kutokana na hali hiyo, ametoa tahadhari kwa wananchi wote kuacha kutumia nyama ambazo hazijapimwa.

"Ugonjwa huu ulizuka tangu Februari 21, mwaka huu, lakini jitihada za makusudi zinafanyika kuudhibiti na hadi kufikia sasa upo katika wilaya tatu za Moshi, Rombo na Siha. Wananchi wa maeneo hayo tunaomba kuzidisha umakini katika ununuzi wa nyama na utumiaji wa
nyama," alisema Mkuu wa mkoa.

Alipotafutwa kuzungumzia hatua za kitaalam zilizochukuliwa kukabiliana na ugonjwa huo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Best Magoma, alisema jitihada za makusudi zinachukuliwa kama kutoa elimu na kuteketeza mizoga yote kwa moto ili kuhakikisha ugonjwa huo hauendelei kuenea wala kuambukiza.

"Ugonjwa huu ni hatari sana na unauwezo wa kukaa chini ya ardhi miaka 100 na mara nyingi umekuwa ukizuka kipindi cha kiangazi, hivyo wananchi wote tupate chanjo za kuzuia ugonjwa huu," alisema Magoma.

Juzi, Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Prof. Philimon Wambura, aliwatahadharisha wananchi kuhusu tishio la kuwapo kwa nyama ya ng'ombe yenye ugonjwa.

Aliwataka wawe makini kwa kuhakikisha wananunua kitoweo hicho kwenye maeneo yaliyosajiliwa nchini.

Vyombo vya habari viliripoti juzi kuwa kutokea kwa vifo vya watu watano na ng'ombe 21 kutokana na ugonjwa huo wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro.

Prof. Marwa alisema ugonjwa huo ni hatari kwa kuwa ng'ombe anakufa ghafla akiwa amenona, hivyo watu wenye tamaa ya fedha wanaweza kuuza nyama hiyo pasipo kujali athari zitakazojitokeza.

"Hatari inaweza kuwakabili zaidi wale wanaopenda kula nyama zisizokaguliwa ambazo haziuzwi kwenye maeneo rasmi yaliyosajiliwa, sasa wabadilike, waache kununua vichochoroni kuepuka shida zinazosababishwa na ugonjwa huo hatari," alisema.

*Imeandikwa na Godfrey Mushi na Mary Mosha.

Habari Kubwa