Waliolipwa fedha korosho kuanikwa

19Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Mtwara
Nipashe
Waliolipwa fedha korosho kuanikwa

WAZIRI wa Kilimo, Japhet Hasunga, ameagiza kubandikwa kwa majina ya wakulima wote waliolipwa fedha za korosho ikiwa hatua ya kuondokana na taarifa potofu zinazotolewa na baadhi yao kuwa hawajalipwa.

Amesema baadhi ya wakulima wamekuwa wakidai kuwa hawajalipwa fedha kutokana na kuuza korosho wakati si kweli na kwamba watu wa namna hiyo wanaichafua serikali.

Hasunga alitoa agizo hilo jana alipokuwa akizungumza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwenye kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.

“Nashangaa sana kila mkulima akiulizwa anasema hajalipwa jambo hili si kweli. Nadhani wanafanya hivi kukwepa madeni wanayodaiana huko vijijini. Sasa naitaka timu ya wataalamu wa Operesheni Korosho kuhakikisha majina yote ya wakulima waliolipwa yanabandikwa kwenye ofisi za vijiji,” alisema.

Katika kutekeleza hilo, aliwataka wataalamu hao kubandika majina ya watu wote waliolipwa na kiasi cha fedha walizolipwa.

“Mpaka sasa tani 222,684 zimekwishakusanywa na hadi Machi 14, mwaka huu, jumla ya Sh. bilioni 596.9 kati ya Sh. bilioni 722 zilikuwa zimeshalipwa kwa wakulima, lakini nashangaa wakulima wanasema hawajalipwa, hii si sawa,” alisema Hasunga.

Waziri Hasunga pia alisema serikali imejipanga hadi Machi 31, mwaka huu, kuwalipa wakulima wote waliobaki kwa kuwa uhakiki umekamilika kwa kiasi kikubwa.

Alisema serikali inapaswa kuungwa mkono kwa uamuzi mgumu iliochukua kwenye korosho kwa kuamua kuwalipa wakulima Sh. 3,300 kwa kila kilo.


Kadhalika, Hasunga alielezea kufurahishwa na mkoa wa Mtwara ambao unazalisha karibu nusu ya korosho zote nchini lakini una idadi ndogo ya wafanyabiashara wa korosho wanaokiuka sheria, maarufu kama ‘kangomba’ kulinganisha na Lindi yenye idadi kubwa.


“Nashangaa sana mkoa wa Mtwara una kangomba 10, lakini ndio wazalishaji wakubwa wa korosho huku mkoa wa Lindi ambao unafuatia kwa uzalishaji wa korosho ukiwa na idadi kubwa ya kangomba ambao wako zaidi ya 400,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Dk. Christine Ishengoma, alimpongeza Waziri Hasunga kwa kuanzisha usajili wa wakulima nchini.

“Nakupongeza sana waziri kwa hili lakini hakikisha unalisimamia kwa weledi ili liwe na matokeo chanya na wakulima kutambulika kote nchini kwa kuwa kufanya hivyo serikali itakuwa na uwezo wa kuwahudumia kwa ufasaha,” alisema.


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, wakiongozwa na Dk. Ishengoma wameanza ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Mtwara kukagua miradi ya maendeleo katika sekta za kilimo, mifugo na maji.

Habari Kubwa