Walionunua madawati 500/- walipa mil. 5.4/-

19Dec 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Walionunua madawati 500/- walipa mil. 5.4/-

SIKU moja baada ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha kuwacharaza viboko wafanyabiashara wa vyuma chakavu waliodaiwa kununua madawati yaliyoibwa shuleni, wamiliki wa biashara hizo wametoa Sh. milioni 5.4 kufidia ya viti vilivyoibwa.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Kenani Kihongosi (kushoto), akimkabidhi Sh. milioni tano na laki nne Mkuu wa shule ya Sekondari Sinoni, Nteles Lorna, kama fidia ya viti vilivyopotea katika shule hiyo baada ya wanafunzi wa shuleni hapo kuviiba viti hivyo na kuwauzia wafanyabiashara wa vyuma chakavu. PICHA: GETRUDE MPEZYA

Desemba 16, mwaka huu, Mkuu wa Arusha aliwacharaza viboko hadharani wafanyabiashara wa vyuma chakavu pamoja na wanafunzi watatu kwa kosa la kuuza viti vya shule kama vyuma chakavu.

Akipokea fedha hizo jana, Mkuu huyo wa wilaya, Kenan Kihongosi, alitoa siku saba kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Sinoni kuhakikisha viti na meza vinapatikana kwa ajili ya wanafunzi wa shule hiyo.

"Mkuu wa shule hizi fedha ndani ya siku saba viti vya wanafunzi viwe vimekamilika na tunajua kiti kimoja ni 50,000 na meza 50,000 jumla ni Sh. 100,000 hivyo jumla ya viti na meza 108 gharama ni 5,400,000," alisema.

Alitoa rai kwa maofisa elimu wilayani hapo kufanya uhakiki wa samani za shule ili kujiridhisha kama kuna madawati ya kutosha wanafunzi kama yalivyotolewa na serikali.

Pia, aliwataka wananchi, wafanyabiashara kuwa wazalendo wa nchi yao na kutoa taarifa sehemu husika ili kuendelea kulinda rasilimali za nchi.

Alisema kuwa baada ya watuhumiwa waliohusika na ununuzi wa vyuma chakavu kukamatwa, waliomba kusamehewa na kuahidi kutoa fedha za kulipa viti hivyo ambapo jana walikabidhi kiasi hicho cha fedha.

Mmiliki wa biashara ya vyuma chakavu, Yuda Kamando, alikiri kuwapo na makosa katika ofisi yake ambapo aliomba kusamehewa na kuahidi kutoa ushirikiano kwa serikali kwa kila hatua.

"Nikiri wazi kuwa kweli ofisi yangu yalijitokeza makosa ya kununua vyuma vitokanavyo na viti vya shule. Mimi sikuwapo lakini vijana wangu walinunua mzigo bila kujua kama bado vilikuwa katika matumizi, ila ninaomba serikali inisamehe na kupitia hili nimejifunza zaidi kwa sasa siwezi kununua chuma ambacho kinaonesha kuendelea na matumizi," alisema Kamando.

Alisema watatoa elimu kwa vijana wanaonunua vyuma ili kuhakikisha wananunua vile vinavyostahili kununua na siyo vinginevyo kwa kuwa kufanya hivyo ni kujiharibia jina katika biashara na kuendelea kujiingiza katika matatizo.

Diwani wa Sinoni, Michael Kivuyo, alisema ni jambo jema wamiliki hao kulipa fedha kwa ajili ya watoto kupata madawati ya kukaa wawapo shuleni kwa kuwa Januari watoto wanapaswa kuendelea kusoma.

"Tunatoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha hususani katika kata yangu ya Sinoni, kuwa walinzi wa mali za serikali ili kuhakikisha hakuna wizi unaojitokeza kwani watoto wamekuwa wakipita mitaani na kuokota vyuma ili kuviuza, tumeshakataa watoto kufanya biashara na badala yake wanatakiwa kusoma," alikumbusha.

Aliwataka wamiliki wa biashara za vyuma chakavu kuacha kununua au kuwatuma watoto kuokota chuma na wakibainika kuendelea kufanya biashara hiyo na watoto, hatua za kisheria zitachukuliwa.

Mmoja wa wazazi wa watoto wanaotuhumiwa kuiba viti hivyo, Saruni Laizer, alishukuru kwa wazazi kusamehewa bila kulipa na kuahidi kutoa ushirikiano wa malezi kati yao na walimu ili kuhakikisha tabia za watoto wao zinakuwa njema.

"Mimi ninalea mjukuu ambaye hana baba wala mama na yupo kidato cha kwanza, nilimpeleka shule kwa lengo la kuja kutukwamua kimaisha mbeleni, lakini matokeo yake ndo haya, kiukweli nimeumia na kuanzia sasa nitahakikisha ninashirikiana na walimu hususani mwalimu wa darasa ili kujenga nidhamu ya mjukuu wangu," alisema Saruni.

Habari Kubwa