Waliopopoa mawe msafara wa DC waiangukia serikali

09Nov 2019
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Waliopopoa mawe msafara wa DC waiangukia serikali

WANANCHI wa Kijiji cha Mpunguti wilayani Kyela mkoani Mbeya, waliouvamia msafara wa Mkuu wa Wilaya hiyo, Claudia Kitta na kuushambulia kwa mawe, wameomba msamaha wakidai walifanya makosa na yanawagharimu.

Waliomba msamaha huo juzi wakati wa ziara ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya iliyokwenda kijijini huko kusikiliza kero za wananchi.

Baadhi ya wananchi hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kyela, Hunter Mwakifuna na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo, Ally Kinanasi, walilazimika kulala kwenye vumbi kuomba wasamehewe.

Mwakifuna alisema kutokana na kichapo walichokipata wananchi wa kijiji hicho kutoka kwa askari wa Jeshi la Polisi, baadhi walikimbia na mpaka sasa hawajarudi na hata walioko, wanaishi kwa wasiwasi wakihofu kukamatwa na polisi.

Alimwomba Mkuu wa Mkoa kuwasamehe wananchi hao kutokana na unyama walioufanya huku akidai kuwa kwa sasa wanashindwa hata kufanya shughuli za maendeleo kijijini huko kutokana na woga huo.

“Mkuu tunaomba utusamehe, tumekosa sana, ni kweli wananchi walipomvamia Mkuu wa Wilaya na wasaidizi wake, tulibaki hatuna namna maana ni kashfa ya aina yake kwetu, tunaomba tusamehe,” Mwakifuna alisema.

Aliongeza kuwa kutokana na tatizo hilo baadhi ya wazazi walitelekeza watoto wao, wakiwamo watoto 19 waliokuwa darasa la saba ambao walikuwa hatarini kutofanya mtihani, kama si jitihada za halmashauri ikishirikiana na viongozi wa dini na kijadi kuhakikisha hawakwami.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kyela, Ally Kinanasi, pia alimwomba Mkuu wa Mkoa kuwasamehe wananchi hao na ikiwezekana hata waliofungwa gerezani kwa kosa hilo nao waachiwe na kurejea kijijini kushiriki shughuli za maendeleo.

Alisema wananchi hao hawana hata uwezo wa kulipa gharama za uharibifu walioufanya kwenye magari ya serikali waliyoyapopoa mawe, hivyo akaomba wananchi hao wasamehewe.

“Sisi kama chama pia tunakuomba upite kwenye kauli ya Rais anayosema ‘anaona huruma sana anapoona watu wapo gerezani’, tunaomba utusamehe na ikikupendeza hata wenzetu waliopo gerezani warejee,” Kinanasi alisema.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei, aliwataka wananchi hao kuepuka kujichukulia sheria mkononi kwa kuwa ni kosa la jinai na litawagharimu.

Alisema magari yote ya serikali ni mali ya wananchi kutokana na kwamba yanaendeshwa kwa kodi zao, hivyo kilichofanywa na wananchi hao ni kujiumiza na kujikosesha huduma.

Akijibu maombi ya wananchi hao, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, alisema amewasamehe wananchi wa kijiji hicho, lakini hana mamlaka ya kuwatoa mahabusi gerezani, hivyo wasubiri uamuzi wa mahakama.

“Kitendo cha kurusha mawe kilinifanya nifikirie kuwa mlidhamiria kuua ama kuuawa, kitendo cha kumvamia askari mwenye bunduki, unataka akuue na mngeuawa, nisingetetea chochote," Chalamila alisema.

Alisema alimwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa kupeleka askari 100 mara ya kwanza na baadaye akaagiza waongezwe hata 200 ili kuwatia adabu wananchi hao.

Habari Kubwa