Walioshinda rufani wachapwa viboko

29Apr 2021
Nebart Msokwa
MBEYA
Nipashe
Walioshinda rufani wachapwa viboko

MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, ameamuru wanafunzi saba kati ya 20 wa Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Iyunga jijini Mbeya waliokuwa wanatuhumiwa kuchoma moja ya majengo ya shule hiyo, kucharazwa bakora tano na kulipa Sh. 300,000 kila mmoja licha ya kushinda rufani zao.

Wanafunzi hao baada ya kufukuzwa shuleni Machi 18, mwaka huu, walikata rufani kwenye Kamati ya Rufani ya Mkoa ambayo iliridhiwa warejee shuleni. 

Chalamila pia ameagiza shule hiyo kuwa chini ya ulinzi wa vyombo ambavyo hajaviweka wazi na kuagiza mwanafunzi yeyote atakayekamatwa nje ya shule muda ambao hauruhusiwi kisheria, akamatwe na kupelekwa 'selo'.

Vilevile, ameliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata wanafunzi wote wanaodaiwa kuvunja maduka na nyumba za walimu na kuiba ili wawajibishwe kwa mujibu wa sheria ili kukomesha vitendo hivyo.

Chalamila alitoa uamuzi huo jana alipoiongoza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo kuitembelea shule hiyo kwa ajili ya kuangalia uharibifu uliofanywa na wanafunzi hao.

Kabla ya Chalamila kutoa uamuzi huo, Mkuu wa Shule hiyo, Edward Mwantimo, alibainisha kuwa baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wamekuwa wakikiuka miiko na taratibu za shule ikiwamo kumiliki simu, kutoroka shuleni usiku na kwenda kuzurura mitaani.

Alibainisha kuwa hivi karibuni walifanya msako na kukamata simu walizokuwa wanazitumia na wanafunzi hao na kisha wakaanza vikao vya kisheria vya shule ikiwamo kikao cha nidhamu kwa ajili ya kushughulikia tatizo hilo.

Mkuu wa Shule huyo aliendelea kubainisha kuwa wakati wanaendelea na vikao hivyo, baadhi ya wanafunzi walichoma stoo ya nidhamu lakini baada ya wenzao kushtuka, walipiga kelele na moto ukadhibitiwa haraka kwa ushirikiano kati ya wanafunzi na walimu.

Alisema wanafunzi hao wamekuwa wakichuna nyaya za umeme na kujiunganishia umeme kwa ajili ya kuchaji simu, hali ambayo imekuwa ikihatarisha majengo ya shule hiyo kuungua.

"Moto huo uliwashwa Machi 10, mwaka huu saa saba usiku na usingedhibitiwa mapema, ungeteketeza madarasa hayo nyuma, ya ofisi ya walimu na mabweni yote.

"Tulifanya jitihada za kuwabaini wahusika na ndipo tukawabaini vijana 20 ambao bodi ya shule iliamua kuwafukuza," Mwalimu Mwantimo alisema.

Kiongozi huyo wa shule alisema baadhi ya wanafunzi huwa wanatoroka nyakati za usiku na kwamba wakati mwingine huwa wanakamatwa na askari wanaokuwa kwenye oparesheni za usiku na wanapohojiwa huwa hawakiri kuwa ni wanafunzi mpaka wanapokuwa wamebanwa.

Ofisa Elimu wa Mkoa wa Mbeya, Majuto Njanga, alisema uamuzi wa kuwafukuza wanafunzi hao ulifanyika Machi 18, mwaka huu lakini saba kati yao, walikata rufani kwenye Bodi ya Rufani ya Mkoa ambayo Mwenyekiti wake ni Mkuu wa Mkoa.

Alisema bodi hiyo iliridhia wanafunzi hao kurejeshwa shuleni kwa masharti ya kugharimia ukarabati wa chumba kilichounguzwa, kucharazwa bakora na kwa wale ambao ni wa madarasa ya mitihani, wamalizie masomo yao wakitokea nyumbani.

Njanga aliutaka uongozi wa shule hiyo kuwaondoa mapema wanafunzi wote wanaokiuka miiko na miongozo ya Wizara ya Elimu ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na tabia zao.

"Mwanafunzi ambaye anatoka nje ya shule ni lazima awe kwenye sare za shule vinginevyo hatufai, ni heri tukawa na wanafunzi wachache wenye nidhamu kuliko kuwa na wengi ambao mienendo yao ni mibovu.

Ninawaomba wanangu mjue kwamba elimu ndiyo mkombozi wenu, ulipewa maelekezo yako peke yako lakini unaweza ukaondoka hapa kwa kuiga makundi," alionya.

Baada ya maelezo hayo, Mkuu wa Mkoa Chalamila aliwaamuru wanafunzi hao kupiga ‘push up’ na akaamuru mmoja wa walimu wa shule hiyo kuwacharaza bakora tano kila mmoja.

"Wa kidato cha nne na sita ambao watakuwa na mitihani hivi karibuni, watafanya mitihani wakitokea nyumbani na kila wanapomaliza mtihani mmoja, watatoka nje ya shule, tutaweka askari wawili getini kwa ajili ya kuwashughulikia watakapogoma kutoka," alisema Chalamila.

Alimtaka Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, William Ntinika, kushirikiana na Mkuu wa Shule hiyo kudhibiti tabia za wanafunzi hao ikiwamo kuwalaza selo na kuwacharaza bakora.

Habari Kubwa