Waliotafuna mabilioni ya Pride kufikishwa kortini

28May 2020
Gwamaka Alipipi
Dodoma
Nipashe
Waliotafuna mabilioni ya Pride kufikishwa kortini

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amesema watu waliojimilikisha viwanja, kula fedha zilizokuwa za Kampuni ya Pride Tanzania, watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, picha mtandao

Waziri Mpango aliyasema hayo bungeni wakati akitolea ufafanuzi wa hoja zilizoibuliwa na wabunge wakati wakichangia taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kuhusu taarifa ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2018/19.

Wabunge hao walitaka majibu ya serikali juu ya kampuni hiyo kudaiwa Sh. bilioni 130.149 zikiwa ni za mikopo kwa taasisi za fedha za ndani na nje ya nchi, amana za wateja, malipo ya bima na watoa huduma wengine.

Pia walilamika kuwapo kwa ubadhirifu wa Sh. milioni 585.935 za malipo ya watoa huduma mbalimbali kwa huduma ambazo hazikufanyika katika kampuni hiyo kwa kipindi cha mwaka 2015 hadi mwaka 2017.

“Mheshimiwa Spika, tumehangaika sana sana na Kampuni ya Pride kama serikali, kwa kipindi kirefu imekuwa ikiendeshwa kinyemela kama kampuni binafsi mpaka Oktoba 2018, ndipo Mahakama Kuu ya Tanzania kupitia Division ya Biashara ndipo ilipotoa uamuzi wa makubaliano kuwa Pride ni mali ya serikali,” alisema Dk. Mpango na kuongeza:

“Pamoja na hatua ambazo serikali imezifanya kuitwaa rasmi Pride, lakini tulihitaji kuhakiki mali na madeni ya Pride na kazi hii imefanyika na imekamilika, serikali hiyo hiyo, ilimwagiza CAG kufanya ukaguzi maalumu ili kuiwezesha kufanya maamuzi yanayostahili,” alisema Dk. Mpango.

Dk. Mpango aliongeza: “Na niliambie Bunge lako tukufu, ukaguzi huo umekamilika na tunaendelea kuichambua hiyo taarifa, ili tuweze kuchukua hatua sahihi ili kuboresha utendaji wa Pride, timu ya wataalamu ndani ya serikali imeundwa na inaendelea na kazi ya kuchambua.”

Alisema: “Mheshimiwa Spika nikuhakikishie kabisa, pamoja na bunge lako kwamba wale wote waliojimilikisha Pride wakala fedha za umma, wakachukua na viwanja hawa tutawashughulikia kwa mujibu wa sheria za nchi.”

Kuhusu Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kufanya operesheni ya maduka ya kubadilishia fedha iliyofanyika mwaka 2018, Dk. Mpango alisema: “Mpaka sasa bado maduka 10 tu ambayo mchakato unaendelea, wakimaliza majadiliano watarudishwa vifaa vyao tukishajiridhisha tuko sawa, shughuli zao zinaendana na maslahi ya taifa.”

Habari Kubwa