Waliouza ardhi msitu Zigua kukiona cha mtemakuni

03Sep 2017
Robert Temaliwa
Nipashe Jumapili
Waliouza ardhi msitu Zigua kukiona cha mtemakuni

ILI kunusuru msitu wa Zigua unaovamiwa mara kwa mara na kutishiwa kutoweka, kuanzia sasa viongozi wa vijiji, kata, vitongoji na wa wilaya za Kilindi na Handeni mkoani Tanga na Bagamoyo mkoa wa Pwani , wawametakiwa kuandaa mikutano ya kuhimiza kuulinda.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga.

Mikutano itafanyika mara kwa mara kwa ajili ya kutoa elimu ya kuhifadhi msitu wa Zigua ambao kwa muda mrefu umekuwa ukivamiwa.

Mwenyekiti wa kamati ya kuondoa wavamizi katika msitu wa Zigua iliyoundwa na wilaya tatu za Kilindi, Handeni na Bagamoyo,

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga, alitoa agizo hilo juzi wakati wa kufunga oparesheni maalum ya kuondoa wavamizi ndani ya msitu huo.

Mwanga alisema kufuatia elimu waliyowapatia watendaji hao wa vijiji, kata na vitongoji wakati wa kuwaondoa wavamizi katika msitu wa Zigua wanapaswa kuitisha mikutano ya hadhara ili elimu hiyo iwafikie wananchi wote wanaozunguuka hifadhi ya msitu huo.

Aidha, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Prof. Dos Santos Silayo, amewataka wale wote waliohamishwa ndani ya msitu huo ambao wanadai waliuziwa maeneo hayo na wenyeviti wa vijiji, kutoa ushirikiano ili wenyeviti waliohusika wachukuliwe hatua za kisheria.

Alisema wale wote waliohusika kuhujumu rasilimali za taifa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ili kukomesha tabia hiyo na kulinda misitu yote nchini.

Prof. Silayo, alizipongeza kamati za ulinzi na usalama za wilaya hizo tatu kwa jitihada ya kuwaondoa wavamizi ndani ya msitu huo.

Alisema hifadhi za misitu hapa nchini zinakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwamo ugumu wa kufikia misitu hiyo jambo ambalo linasababisha wavamizi kuingia wakiona kama ni mapori ambayo hayana wenyewe.

Alisema kwa sasa wakala wa huduma za misitu Tanzania umejipanga kuilinda misitu yote na kwamba ulinzi huo utakuwa shirikishi na endelevu.

Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa opesheni hiyo ya kuondoa wavamizi ndani ya msitu wa Zigua, mkaguzi msaidizi wa zimamoto, Henry Mwaluseka, alisema jumla ya nyumba zilizobomolewa katika uondoaji huo ni nyumba 62 za bati , za nyasi 863, mazizi ya mifugo 112 na maghala ya asili 19.

Mwaluseka alisema katika operesheni hiyo mazao ya muda mfupi yaliyopandwa ndani ya msitu hayakuharibiwa na badala yake wahusika wamepewa muda ili wavune na kusisitizwa kutorudia kufanya shughuli za kilimo na shughuli nyingine zote za kibinadamu ili kuuacha huru msitu huo uweze kurudisha uoto wake wa asili na kuhifadhi vyanzo vya maji na wanyama wanaoishi humo.

Msitu huo wa Zigua una jumla ya hekta 24, 436 ukiwa na urefu wa kilomita 172 ambao umepakana na Wilaya za Bagamoyo, Handeni na Kilindi.

Bagamoyo sehemu kubwa ya msitu huo inapatikana kata ya Kibindu katika Halmashauri ya Chalinze.

Habari Kubwa