Waliovamia hifadhi ya shule watangaziwa vita

03Sep 2017
Steven William
Nipashe Jumapili
Waliovamia hifadhi ya shule watangaziwa vita

BAADHI ya wananchi waliovamia na kujenga nyumba eneo la Shule ya Msingi Mtindiro wilayani Muheza mkoa wa Tanga, wametakiwa kuondoka wenyewe kabla ya kupelekwa mahakamani.

Mkuu wa Wilaya, Mwanasha Tumbo.

Aidha, wameagizwa kuondoka mara moja kupisha eneo la shule hiyo kabla hawajapelekwa mahakamani, amri ikitolewa na Mkuu wa Wilaya, Mwanasha Tumbo alipotembelea shule hiyo juzi.

Tumbo alikwenda Mtindiro baada ya kupata taarifa kwamba kuna watu wamevamia eneo la shule hiyo na kujenga nyumba .

Mkuu huyo wa wilaya alifika shuleni hapo akitokea katika kikao cha kujadili ugawaji wa mashamba ya mkonge ya Lewa Estate
na Sagulas Estate kwa wakazi wa kata ya Kwabada na Mtindiro ambayo yamefutiwa hati na Rais John Magufuli, na sasa yatagawanywa kwa wananchi.

Alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Muheza Luiza Mlelwa, kutoa maelekezo kwa Ofisa Ardhi wilayani Salehe Kamnge, kupima eneo hilo la shule na kujua hifadhi yake.

Tumbo alipiga marufuku wananchi kuvamia maeneo ya taasisi zote za serikali kwani kufanya hivyo ni kosa linaloweza kuwapeleka mahakamani.

Mkurugenzi Mlelwa alisema kuwa atahakikisha anafuatilia mipaka ya shule ili watu waliovamia kujenga katika eneo waondoke.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Muheza Peter Jambele, aliunga mkoono maelekezo ya Mkuu wa Wilaya kwamba ni lazima sheria ichukuwe mkondo wake watu ambao wanajenga kwenye ardhi za shule na vituo vya Afya.

Habari Kubwa