Waliozozania SUA wasuluhishwa

23Feb 2021
Ashton Balaigwa
Morogoro
Nipashe
Waliozozania SUA wasuluhishwa

MGOGORO wa muda mrefu wa kugombania Shule ya Sekondari ya SUA, kati ya kata ya Mbuyuni na ya Magadu katika Manispaa ya Morogoro, umemalizika kwa kila kata kupewa kazi ya kujenga madarasa.

Katika mvutano huo wa siku nyingi ambao, kila kata ilidai kuwa shule hiyo ni mali yake, ulitatuliwa kwa namna tofauti na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare, kuwatwisha  mzigo  watendaji wa mitaa ya kata hizo  kujenga vyumba vitano vya madarasa ndani ya mwezi mmoja.

Uamuzi wa Ole Sanare, umekuja baada ya kuzuru kata hizo na kushuhudia kuwa hakuna ujenzi wa madarasa, kwa kisingizio kuwa hafahamiki mmiliki halali wa sekondari ya SUA.

Baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili na kujiridhisha, Mkuu wa Mkoa alieleza kuwa mvutano huo hauna tija kwa wanafunzi wanaohitaji kuingia madarasani yanayotakiwa kujengwa haraka ili waanze masomo.
Aliwaagiza watendaji wa mitaa wa kata zote mbili kusimamia ujenzi huo.

Katika maagizo yake alitoa mwezi mmoja kujenga vyumba vitano vya madarasa pembeni mwa majengo ya shule, lakini ndani ya eneo lake ili kukamilisha haraka kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madarasa katika shuleni hapo.

Ole Sanare, alisema Kata ya Mbuyuni yenye mitaa sita itajenga vyumba viwili wakati Magadu yenye mitaa tisa itajenga vyumba vitatu vya madarasa na kuwezesha kupatikana vyumba vitano.

“Natoa mwezi mmoja kwa kila kata kujenga vyumba hivyo tulivyowapangiana na vifikie usawa wa linta. Ninataka yakikamilika mumkabidhi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ili kuyamalizia,” alisema.

Kuhusu mvutano uliokuwapo, mkuu huyo wa mkoa aliwataka viongozi wa pande zote mbili kukubaliana  kujenga madarasa hayo matano mbali kidogo na majengo ya sasa ya shule hiyo na yatakapokamilika siku zijazo kupitia majengo hayo wanaweza kuamua kuifanya shule inayojitegemea, hivyo kila kata kuwa na shule yake na kuondoa mvutano uliokuwapo.

Diwani wa Kata ya Mbuyuni, Samwel Msuya, alisema changamoto iliyokuwapo katika ujenzi wa sekondari ya SUA, ni baada ya kata yake ya Mbuyuni kushtakiwa na kukatazwa kuendeleza shule hiyo, hali iliyosababisha kudorora kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Msuya alisema hadi sasa changamoto hiyo imekwishatatuliwa na wananchi wa Mbuyuni na Magadu wapo tayari kuendeleza ujenzi wa madarasa katika shule hiyo.

Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Pascal Kihanga, alisema, umiliki wa shule hiyo iwe ya nani siyo muhimu kwao.

Aliwaambia kinachotakiwa ni kujenga madarasa ili watoto waliokosa nafasi ya kusoma waingie madarasani na kuanza kusoma na kwamba wahusika wakuu wa kujenga madarasa hayo ni wenye watoto ambao ni wazazi wanaoishi katika kata hizo.

Aliwataka washirikiane kutekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa la kujenga madarasa hayo matano. 

Habari Kubwa