Walipana posho za safari kila siku, mwaka mzima

15Apr 2019
Sanula Athanas
Dodoma
Nipashe
Walipana posho za safari kila siku, mwaka mzima

MDHIBITI na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad, amebaini matumizi mabaya ya fedha kwenye Tume ya Huduma za Walimu, ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wake kulipwa posho za kuwa safarini kila siku kwa mwaka mzima. 

MDHIBITI na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad, picha mtandao

Katika ripoti yake ya ukaguzi ya mwaka 2017/18 iliyowasilishwa bungeni na serikali Jumatano iliyopita, CAG Assad anasema amebaini wafanyakazi mbalimbali wa tume hiyo walilipwa posho inayofikia Sh. milioni 721.05 kwa lengo la kutekeleza shughuli za ofisi.

Anabainisha kuwa tume hiyo imewalipa wafanyakazi posho ya safari kwa siku 324, posho ya kazi za ziada kwa siku 365 na posho za vikao kwa siku 127. 

"Hii si kwamba inaashiria matumizi yenye shaka, bali kutokuwa na uhakika kama wafanyakazi walikuwa nje ya kituo cha kazi kwa mwaka mzima, wakati rejista ya mahudhurio imeonyesha wafanyakazi hao walikuwapo ofisini kwa kipindi hicho.

"Ni mtazamo wangu kwamba, upungufu huu umesababishwa na udhibiti wa ndani na uaminifu hafifu juu ya kulinda na kutumia fedha za umma, ambapo kama hatua hazitachukuliwa, yanaweza kuchochea matumizi mabaya ya fedha za umma.

"Kwa sababu ya udhaifu ulioibuliwa hapo juu, nashauri menejimenti ya Tume ya Huduma za Walimu kuanzisha mifumo imara ya udhibiti wa ndani ikiwamo huduma za ukaguzi wa ndani, yenye vitendea kazi vya kutosha na mgawanyo imara wa majukumu ambao unaweza kuwa na umuhimu katika kupunguza vihatarishi vilivyotambuliwa.

"Nashauri zaidi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuchunguza kwa ukaribu suala hili, na itakapohitimishwa wahusika watapaswa kuwajibika," Prof. Assad anatahadharisha katika ripoti yake hiyo.

CAG Assad pia anabainisha kuwa ukaguzi wake ulibaini dosari kwenye matumizi ya Sh. bilioni 4.665 yaliyofanywa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kwenda kampuni binafsi za kisheria bila kufuata makubaliano ya mkataba na upungufu katika usimamizi wa ankra za matibabu nje ya nchi Sh. bilioni 7.013.

Katika ripoti hiyo, CAG Assad anabainisha utata wa miamala iliyofanywa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime Sh. milioni 514, ongezeko la gharama za kukodi magari katika balozi za Tanzania zilizoko Moroni na Brasilia Sh. milioni 87.461, malipo yasiyo na vithibitisho Sh. bilioni 4.369, Kodi ya Zuio ambayo haijadaiwa Sh. milioni 722.173, malipo yasiyokuwa na risiti za kielektroniki (EFD) 
Sh. bilioni 1.432.

Habari Kubwa