Wamachinga waongezewa siku 12 Dar, Samia apongeza

19Oct 2021
Maulid Mmbaga
Dar es Salaam
Nipashe
Wamachinga waongezewa siku 12 Dar, Samia apongeza

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, ameongeza siku 12 kwa wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama machinga kujiandaa kuhamia maeneo waliyotengewa ili kuepuka usumbufu na kurahisisha usafi wa mji.

Amesema baada ya muda huo hatasikiliza kisingizio chochote kutoka kwa wafanyabiashara hao, zaidi ya kuhamia wanakotakiwa na kuondoka kusikotakiwa.

Akizungumza jana na wafanyabiashara katika Soko Kuu la Kariakoo, alisema uamuzi huo umekuja baada ya mwezi mmoja uliotolewa kujiandaa na kuondoka katika maeneo yasiyo rasmi kuisha.

“Nawapa muda mpaka Oktoba 30, baada ya hapo sitaki kusikia kisingizio chochote labda mtu aje na malalamiko kwamba kaenda kwenye maeneo yaliyotengwa kakosa nafasi, wanaotakiwa kuondoka ni wale walio juu ya mifereji na mitaro, hifadhi za barabara na mbele ya shule au taasisi za serikali,” alifafanua.

Pia alisema watajadiliana na uongozi wa wafanyabiashara hao na kusisitiza kuwa serikali inawathamini ndiyo maana wametengewa maeneo, kwa mpango wa muda mrefu ni kuliweka jiji hilo kuwa mfano wa kuigwa kwenye usafi barani Afrika.

Aidha, aliagiza eneo la DDC, Kariakoo liboreshwe ili kupokea wafanyabiashara wengi zaidi tofauti na sasa linapotumika kuuza vyakula na vinywaji.

Mkuu huyo wa mkoa alisema ameridhishwa na baadhi ya wafanyabishara hao kuhama kwa hiari maeneo wasiyotakiwa.

Makalla alisema hadi sasa maeneo ambayo wafanyabiashara wameondoka na kufanikiwa kuwa wazi ni Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Maktaba Posta, Vingunguti, Gongolamboto, Mikocheni na Mwenge, na kwamba japokuwa baadhi ya maeneo mama lishe wanaonekana kuvunja vibanda, lakini wakiendelea na biashara kwa kuweka mwamvuli.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Machinga, Steven Lusinde ameiomba serikali kuwapeleka kwenye maeneo yaliyo na mwingiliano mkubwa wa watu kuliko na biashara.

“Tunaiomba mamlaka kutekeleza amri kwa makubaliano kwani wafanyabiashara wengi wanayo mikopo na wanategemewa na watoto ikiwa ni pamoja na kukidhi mahitaji yao,” alisema.

Pia, inasadikika kuwa zaidi ya wafanyabiashara 5,000 wataathirika na uamuzi wa mamlaka za miji kwa kuwaondoa maeneo yasiyo rasmi.

Katika Soko la Kariakoo ambako wafanyabiashara zaidi ya 1,500 wanaendesha shughuli zao na kujiingizia kipato kinachowasaidia kumudu gharama za maisha, walisema wanahitaji kuwa na uhakika wa biashara yao katika soko hilo linalohudumia zaidi ya watu 3,000 kwa siku.

Hivi karibuni, akihutubia wakazi wa Jiji la Arusha, Rais Samia Suluhu Hassan, aliipongeza Dar es Salaam kwa kuwapanga machinga kiasi cha kuwezesha maeneo mengi kuonekana vizuri na kurahisisha usafi na kuwataka miji na majiji mengine kuiga.

Habari Kubwa