Wambura alifikishwa viunga vya Mahakama hiyo leo Februari 11, 2019 mapema saa 5:48 asubuhi na kupandishwa kizimbani saa 6:45 mchana.
Kigogo huyo wa mpira alisomewa mashtaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Kelvin Mhina.
Upande wa Jamhuri uliongozwa na Mawakili wa Serikali George Barasa, Moza Kasubi na Imani Mitumizizi.
Barasa alidai kuwa mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka 17.
Katika shtaka la kwanza ilidaiwa kuwa Julai 6, 2004 mahali pasipojulikana jijini Dar es Salaam, akiwa na nia ya kutapeli alighushi barua yenye jina la E.Maganga Mtandaji Mkuu wa Kampuni ya Jeck System Ltd.
Ilidaiwa kuwa mshtakiwa alighushi barua hiyo akidai TFF irejeshe mkopo wa Dola za Marekani 30,000 kwamba alilikopesha shirikisho hilo huku akijua ni uongo.
Shtaka la pili, Julai 6,2004 Wambura aliwasilisha TFF nyaraka ya kughushi akionyesha kwamba barua hiyo imeandikwa na E.Maganga mtendaji Mkuu Kampuni ya Jeck System Ltd kuwa alilikopesha shirikisho hill Dola za Marekani 30,000.
Katika shtaka la tatu mpaka la tano, Juni 17, Agosti 19 na Julai 31, 2015 ofisi za TFF zilizopo Ilala, jijini Dar es Salaam,mshtakiwa alijipatia Sh.milioni 14 kama malipo ya mkopo na riba ya Dola za Marekani 30,000 huku akijua ni uongo.
Kasubi alidai katika shtaka la sita mpaka la 10, katika tarehe tofauti ofisi za TFF, mshtakiwa alijipatia Sh.61,902,200 kama malipo ya mkopo na riba ya Dola za Marekani 30,000 huku akijua ni uongo.
Jamhuri uliendelea kudai kuwa katika shtaka la 11 mpaka la 15, katika tarehe tofauti ofisi za TFF, mshtakiwa alijipatia Sh. 35,095,424 kama malipo ya mkopo na riba ya Dola za Marekani 30,000 huku akijua ni uongo.
Shtaka la 16, ilidaiwa kuwa kati ya Agosti 15 na Oktoba 21, 2014 katika ofisi TFF mshtakiwa alitakatisha Sh. 25,050,000 kutoka katika shirikisho hilo wakati akijua fedha hizo ni zao la kughushi.