Wambura mahabusu bado yamhusu

24May 2019
Hellen Mwango
DAR
Nipashe
Wambura mahabusu bado yamhusu

MAKAMU wa Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura, ataendelea kukaa mahabusu baada ya kesi yake kuahirishwa kwa mara nyingine hadi Juni 4, mwaka huu.

 Kesi hiyo ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha iliahirishwa baada ya upande wa Jamhuri kudai kuwa upelelezi bado haujakamilika.

Jana kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Kelvin Mhina.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo kuomba  tarehe nyingine ya kutajwa.

Hakimu alisema kesi hiyo itatajwa tena Juni 4, mwaka huu na mshtakiwa ataendelea kukaa mahabusu.

Katika kesi ya msingi, kigogo huyo wa mpira wa miguu anakabiliwa na mashtaka 17, yakiwamo ya kughushi, kutoa na kuwasilisha nyaraka za uongo,  mashtaka 13 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na  mawili ya kutakatisha fedha haramu.

Katika shtaka la kwanza ambalo ni la kughushi, mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Julai 6, 2004, sehemu isiyojulikana ndani ya jiji la Dar es Salaam.

Ilidaiwa kuwa Wambura kwa nia ya kutapeli, alitengeneza barua ya kughushi ambayo haina kumbukumbu namba akionyesha imeandikwa na E. Maganga ambaye ni Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Jeck System kuwa anadai kurejeshewa malipo ya mkopo wa USD 30,000 pamoja na riba aliyokuwa ameikopesha TFF.

Katika shtaka la kutoa na kuwasilisha nyaraka ya uongo, mshtakiwa anadaiwa kutoa  barua iliyokuwa haina kumbukumbu namba ya Julai 6, 2004, akijifanya kwamba ni barua iliyoandikwa na E. Maganga ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Jeck System Ltd, akionyesha kuwa anadai mkopo wa USD 30,000 pamoja na riba waliokopeshwa TFF huku akijua kuwa siyo kweli.

Pia katika mashtaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, Wambura anadaiwa kutenda kosa hilo, Juni 17, 2015 katika ofisi za TFF, ambako kwa njia ya udanganyifu, alijipayia Sh. Milioni 10 kutoka TFF kwa kuonyesha kuwa ni sehemu ya malipo ya Dola za Marekani 30,000 pamoja na riba kutoka kwenye kampuni ya Jeck Systam  jambo ambalo si kweli.

Katika shtaka la utakatishaji fedha, Wambura anadaiwa kati ya Agosti 15 na Oktoba 21, 2014, makao makuu ya TFF alijipatia Sh. Milioni 25 kutoka TFF huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la kughushi.

Habari Kubwa