Wamiliki baa wafurahia wazo la Makonda

06Jan 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Wamiliki baa wafurahia wazo la Makonda

SIKU moja baada ya Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Paul Makonda, kusema shauku yake ni kuona wafanyabishara wa mkoa huo, hususani baa kufanya kazi saa 24, wamiliki hao wamempongeza na kumwomba aharakishe utaratibu huo.

Maoni ya wamiliki wa baa jijini Dar es Salaam baada ya kusikia mtazamo wa mkuu wa mkoa wa jiji hilo juu ya shauku ya kuona wafanyabiashara wakifanya kazi masaa 24.

Wamiliki wa baa wamemwomba Makonda apitishe uamuzi huo ambao utakuwa na manufaa kwa wamiliki na utawezesha serikali kupata mapato ya kutosha.

 

Wakizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, baadhi ya wamiliki hao walisema mpango wa Makonda ni wa kupongezwa na kuungwa mkono kwa sababu moja ya changamoto zilizokuwa zikiwakera wafanyabiashara wa vinywaji ni kufunga ofisi saa 6:00 usiku.

 

“Leo (jana) niliposikia alichosema Makonda, nilifurahi sana nikasema amefanya jambo jema linalopaswa kuungwa mkono kwa sababu wafanyabiashara tulikuwa tukikosa fedha kwa sababu hakuna muda wa kutosha kufanya biashara,” alisema mmoja wa wafanyabishara eneo la Sinza, John Haule.

 

Naye Meneja wa baa ya The Great Park iliyoko Tabata Barakuda, Shaban Juma, aliunga mkono mpango huo  akisema kwa muda muda mrefu wamekuwa wakishindwa kufanya biashara kwani wateja wake wengi kufika baa kuanzia saa 4:00 usiku.

 

“Alichosema Makonda ni jambo zuri sana. Tulikuwa tunashindwa kufanya biashara kwa sababu wateja wengi wanaingia baa kuanzia saa 4:00 usiku wakitokea kazi na ikizingatiwa kuwa barabarani kuna foleni, hivyo hawakai vizuri. Saa 6:00 inafika na wanaanza kufukuzwa,” alisema Juma.

 

Alisema suala la ulinzi haliwezi kuwa shida kwani kuna askari wa kutosha kuimarisha usalama kwa sababu wamekuwa wakizunguka usiku kucha na magari yao kufukuza wanaokaa baa.

 

Naye Meneja wa baa ya Forty Forty Tabata, Mohamed Ally, alisema amepokea kwa furaha wazo la Makonda kwa sababu wamiliki na wafanyabishara walikuwa hawana uhuru.

 

Alisema changamoto kubwa iliyokuwa ikiwakabili ni wateja kukamatwa na kuwekwa ndani, wateja kukimbia na fedha, wafanyakazi kukamatwa na mmiliki kuingia hasara ya kuwatoa vituo vya polisi watu waliokamatwa.

“Ni changamoto nyingi zinatukabili wafanyabishara wa bia, kama wakiruhusu tufanye kazi kwa saa 24 tutafanya kwa uhuru zaidi,” alisema Ally.

 

Aliongeza kuwa, licha ya Makonda kuongeza muda hadi saa 8:00 usiku badala ya saa 6:00, askari polisi wamekuwa wakiwakamata wateja wao inapofika saa 6:00 usiku.

 

“Askari wanakuja saa 6:00 usiku na kuanza kututishia na unapowahoji wanasema hawatambui wanachofahamu saa 6:00 baa zifungwe, hivyo wanaanza kutulazimisha kufunga, wateja wanakimbia hovyo,” alisema.

 

Alisema kutokana na changamoto hizo, wamiliki wa klabu zinazokesha (night clubs) wamekuwa wakilazimika kuwarundika wateja wao kwenye kumbi hizo ili kukwepa kukamatwa inapofika saa 6:00 usiku.

 

Pia alisema usalama wa baa hizo si tatizo kwa sababu vyombo vya ulinzi na usalama vimekuwa vikizunguka kwenye maeneo mengi ya Jiji hilo usiku.

 

Naye Meneja wa baa ya Highburry Kings, Tabata Mawenzi, Godfrey Mallya, alisema wamiliki na wafanyabishara wa baa wangefurahi kama wangefanya kazi kwa saa 24.

 

“Asubuhi nilipoamka nilienda kusoma gazeti la Nipashe nijue alichosema Makonda. Ni jambo jema kama ataruhusu tuuze vinjwaji wakati wote, tutapata fedha za kutosha, kodi tutalipa na usalama upo wa kutosha,” alisema Mallya.

 

Alisema pia kama mteja akiruhusiwa kunywa kinywaji wakati wa mchana anapomaliza kula chakula ni jambo jema kwa sababu watu wote si watumishi wa umma wala wafanyakazi wa ofisini.

 

“Wafanyabishara wa vinyaji hatupati faida kwa sababu hakuna biashara, watu wanaokuja kunywa supu au kula chakula tunashindwa kuwauzia vinywaji kwa sababu serikali imekataza hadi kuanzia jioni wakati watu wengine si watumishi wa maofisini, kama wakiruhusu tutafurahi sana,” alisema Mallya.

 

Naye msambazaji wa vinywaji katika baa mbalimbali kutoka kampuni ya Mabibo Wines and Spirits, Derick Chezzy, alisema hiyo ni habari njema kwa wafanyabishara na wasambazaji wa vinywaji kwa sababu watu watakuwa na uhuru wa kunywa na serikali itapata fedha za kutosha kutokana na kodi.

Kuhusu suala la usalama, alisema magari ya doria na askari wapo wa kutosha wanaoweza kudhibiti uhalifu na hawaoni changamoto inayosababisha kutekelezwa kwa jambo hilo.

 

Naye mkazi wa Kimara, Amani Chaurembo, aliieleza Nipashe kuwa wanywaji wa bia wamekuwa wakikosa uhuru wanapokuwa baa kwa sababu askari wamekuwa wakiwakamata na wanapofikishwa kituo wanatakiwa kulipa fedha.

 

“Nafikiri watu wapewe uhuru, sheria na taratibu za nchi zifuate hakuna atakayevunja sheria. Hii tabia ya askari kukamatwa watu waliokaa wanakunywa vinywaji kwa starehe zao siyo vizuri tunakuwa kama wakimbizi,” alisema Chaurembo.

 

Kuhusu usalama, alisema nguvu inayotumika kukamata watu wanaokunywa wakiwa baa kuanzia saa 6:00 usiku ielekezwe kwenye kulinda usalama wa raia na mali zao wakiwa wanakunywa vinywaji.

 

Juzi Mkonda akizungumza na vyombo vya ulinzi na usalama, wakuu wa wilaya, makatibu tawala, maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa huo, kuhusu mkakati wa kukusanya mapato bila kuwabughudhi wafanyabishara, alisema kwa sasa baa zinafanya kazi hadi saa 8;00 usiku lakini lengo lake zifanye kazi kwa saa 24.

 

“Maana ya jiji la Dar es Salaam kuwa jiji la kibiashara ni pamoja na kuwawezesha wafanyabishara kufanya kazi kwa saa 24. Kwa sasa baa zinafunguliwa hadi 8:00 usiku lakini mpango wetu zifunguliwe muda wote ili serikali ipate mapato,” alisema Makonda.

 

 

 

Habari Kubwa