Wamiliki maduka ya fedha Arusha wamwangukia Samia

09May 2022
Na Waandishi Wetu
Arusha
Nipashe
Wamiliki maduka ya fedha Arusha wamwangukia Samia

WAFANYABIASHARA wa maduka ya kubadilisha fedha jijini Arusha, wanaiomba serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuingilia kati ili warudishiwe mali zao na kuwajengea mazingira rafiki, ili waendelee na shughuli hiyo bila vikwazo.

Maombi ya wafanyabiashara hao kwa mkuu wa nchi ni pamoja na kuwarudishiwa fedha, leseni na mali zao zilizochukuliwa wakati wa kufungwa kwa maduka yao na mamlaka za serikali Novemba, mwaka 2018. 

Hata hivyo, wameishukuru serikali kwa kuwarudishia simu zao za kiganjani na hati za kusafiria zilizokuwa zimechukuliwa tangu wakati huo.

Akizungumza na Nipashe, mmoja wa viongozi wa wafanyabiashara hao, Melance Kisoka, alisema baada ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, kulieleza Bunge kuwa walisharudishiwa vitu vyao, lakini walichorudishiwa ni simu na hati za kusafiria pekee.

"Kwa kweli leseni zetu na fedha zetu, mali zingine kama nyumba na magari hazijarudishwa kwetu na hatujui sababu," alisema.
 
Alisema  pia hata serikali ikiwarudishia fedha zao kwa sasa wengi wao watashindwa kuendelea na biashara hiyo kwa sababu ya ongezeko la mtaji wa kuanza biashara hiyo kuongezwa kutoka Sh. milioni 300 hadi Sh. bilioni moja.
 
Kisoka alisema mwaka 2015 mtaji kwa mtu aliyetaka kuingia biashara hiyo ulikuwa usipungue Sh. milioni 40 na baada ya hapo inapanda hadi Sh. milioni 100 ambayo ilikuwa mwisho wa kuilipa mwaka 2017.
 
"Sasa kabla hata ya tarehe ya mwisho iliyopangwa tuwe umelipa mwaka huo ukapandishwa hadi Sh. milioni 300 na wakati tumeanza kulipa hapo katikati tukavamiwa kwenye maduka yetu na kunyang'anywa, fedha, simu, hati za kusafiria na leseni, huku baadhi wakichukuliwa magari na nyumba zao nangari leo serikali haijarudisha,"alisema.
 
 Alisema wanaiomba serikali iwarudishie mali zao hizo ili waendelee na maisha mengine.
 
Hata hivyo, alisema maridhiano juu ya usalama wa kuanzisha upya maduka hayo ni muhimu, kwa kuwa ni muhimu kuhakikishiwa usalama wa biashara zao ili yasijirudie yaliyojitokeza mwaka 2018. 

"Hapa tunaomba tuhakikishiwe usalama na juu ya kuheshimu sheria za uanzishwaji wa maduka haya kama hawatatuvamia tena ili turejeshe imani kwa serikali," alisema.

Naibu Waziri Masauni, alisema bungeni kuwa wafanyabiashara hao warudishiwe vitu vyao ili wafungue maduka hayo, lakini hadi sasa wengi wameshindwa kufungua. 

SERIKALI WARUSHIANA ‘MPIRA’

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo, alipotafutwa na Nipashe Alhamisi iliyopita alisema hana mamlaka ya kuzungumzia suala hilo na kutaka itafutwe Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa sababu ndiyo inayohusika na maduka ya fedha.
 
Meneja Msaidizi Idara ya Uhusiano wa Umma kutoka BoT, Vick Msina, alipotafutwa kujua nini kinaendelea kuhusiana na fedha na mali za  wafanyabiashara hao alisema kuwa aliyeongoza operesheni hiyo ni DPP (Mkurugenzi wa Mashtaka) hivyo aulizwe yeye.

Gazeti hili lilipomtafuta DPP, Sylvester Mwakitalu, alisema hafahamu chochote mpaka afuatilie kujua majalada hayo yakoje.

“Labda nifuatilie sina taarifa yawezekana majalada yapo lakini sijapata kuyaona,” DPP Mwakitalu aliomba.

Habari Kubwa