Wamiliki viwanja 20,000 hatarini kunyang'anywa

03Dec 2018
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Wamiliki viwanja 20,000 hatarini kunyang'anywa

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi, ametoa mwezi mmoja kwa wamiliki wa viwanja vya miradi maalum ya viwanja 20,000 kuhakikisha wanaviendeleza, vinginevyo serikali itavichukua bila fidia.

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi.

Viwanja hivyo ni vilivyotolewa kwa wananchi katika maeneo maalum miaka 10 iliyopita.Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Lukuvi alisema:

"Miradi hii ilitolewa miaka 10 iliyopita, inaitwa miradi maalum ya viwanja 20,000, ilisimamiwa na wizara hii.

"Ilitekelezwa katika maeneo ya Kibada, Geza Ulole, Mwongozo, Buyuni, Mwanagati, Mbweni Malindi, Mbweni JKT, Mbweni Mpiji, Bunju na Twangoma.“Lakini tumebaini kwamba viwanja hivi zaidi ya asilimia 50 havijajengwa na wala havijatembelewa na watu ambao walivinunua na niliunda timu ambayo ilibaini baadhi ya viwanja viliwekwa majina bandia, vingine havina wenyewe na wengine walinunua pengine wamesahau.

"Nimewaagiza maofisa ardhi wafanye uchunguzi, mwenye kiwanja, yeyote ambaye atakuwa hata hajajenga fensi ya ukuta ifikapo mwisho wa mwezi wa Desemba, hatua za kunyang’anya zianze kuchukuliwa."

Alisema wamebaini wafanyakazi waliopima viwanja hivyo walizuia viwanja vingi na kuweka majina ambayo mengine wameyasahau na kwamba endapo kutabainika viwanja ambavyo viliwekwa na maofisa ardhi vitauzwa na hatua nyingine zitachukuliwa.

Lukuvi pia alisema zaidi ya hati 6,000, zote za Mkoa wa Dar es Salaam zimetelekezwa wizarani na wamiliki wa ardhi ambao waliziomba na zilipotolewa hawakujitokeza kuzichukua.

Alisema baadhi ya watu wanatelekeza hati hizo, ili kukwepa kodi na kwamba watahakikisha wanawapata.

"Kuna hati zaidi ya 6,000 ambazo kwa makusudi watu hawaji kuzichukua na zote ni za Dar es Salaam, nimeagiza maofisa wazichukue na kwenda kuangalia hao watu wapo au hizi hati zilitayarishwa tu na watu wa wizarani hapa kwa namna fulani fulani, lakini kule kwenye ‘site’ kuna majina ya watu wengine? Tunataka kufahamu," Lukuvi alisema.

Habari Kubwa