wamiliki wa makampuni watakiwa kutangaza utalii

02May 2021
Na Mwandishi Wetu
Mwanza
Nipashe Jumapili
wamiliki wa makampuni watakiwa kutangaza utalii

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja, ametoa wito kwa Wafanyabiashara na wamiliki wa Makampuni mbalimbali hapa nchini kuunga mkono juhudi za Serikali za kutangaza utalii na vivutio mbalimbali vilivyopo nchini kupitia biashara zao.

Mary ametoa wito huo leo Jijini Mwanza, wakati wa maonesho ya biashara, uwekezaji na utalii yanayowahusisha wadau mbalimbali, ambapo amesema wafanyabiasha ni wadau wakubwa wa utalii hivyo wana nafasi kubwa ya kuutangaza utalii ili kusaidia kuongeza idadi ya Watalii.

“Nawaomba sana ninyi wafanyabiashara, kupitia makampuni yenu mtangaze utalii wa Tanzania na vivutio vyake, ninyi ni wadau wakubwa wa utalii”  amesema Mary.

Aidha, amewaeleza wafanyabiashara hao kuwa wanapaswa kutambua kuwa sera ya Tanzania ya viwanda itaendelea kutekelezwa kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amekua akiwasisitiza Watanzania wawekeze katika miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki  ambaye ni mgeni rasmi katika tukio hilo amesema wafanyabiashara wakishirikiana vizuri wataweza kukuza uchumi wa nchi pia kuutangaza utalii.

“Serikali tunaendelea kuziondoa changamoto zote zinazolalamikiwa na wafanyabiasha na wawekezaji, tuvute subira kidogo haya mambo yatakwenda kurekebishwa vizuri” amesema Mashimba.

Habari Kubwa