Wamtaka Waziri Jafo kusuka au kunyoa

14Nov 2019
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Wamtaka Waziri Jafo kusuka au kunyoa

CHAMA cha National League for Democracy (NLD) kimetangaza rasmi kujitoa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, huku kikimtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, ajiuzulu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, picha mtandao

Uamuzi wa chama hicho umeongeza idadi ya vyama vya siasa vya upinzani vilivyofikia uamuzi wa kujitoa kushiriki uchaguzi huo kufikia vinane. Vingine ni ACT-Wazalendo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chauma, NCCR-Mageuzi, UPDP, Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Kijamii (CCK).

Kwa mujibu wa taarifa ya NLD iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa chama hicho, Oscar Makaidi, kinamtaka Jafo kujiuzulu mara moja kwa madai kuwa ameshindwa kusimamia uchaguzi huo na kulitia taifa hasara.

“NLD hatuna imani naye licha ya kuagiza kuwa wagombea wote walioenguliwa, warudishwe, agizo ambalo hana mamlaka nalo kikanuni wala kisheria," Makaidi alisema.

Katika taarifa yake hiyo, NLD kimeamua kujitoa katika uchaguzi huo kwa kuwa una kasoro kubwa na haziwezi kurekebishika katika muda uliobaki.

Chama hicho kimemwomba Rais John Magufuli kusitisha uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 24 na mchakato wake wote uanze upya.

“Kwa kuwa Tamisemi imeshindwa kusimamia uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa, tunataka usimamiwe na tume huru ya taifa ya uchaguzi,” alisema.

Makaidi pia alisema NLD haikubaliani na uamuzi wa Jafo kuwa amefuta uamuzi wote uliofanywa na wasimamizi wasaidizi kwa kuwa hana mamlaka hayo kikanuni na kisheria.

“Tunaamini kwamba kuendelea na uchaguzi chini ya usimamizi ule ule ni kuhalalisha upungufu wote uliojitokeza, mwingi ukiwa ni wa makusudi.

"Kuendelea na uchaguzi huu ni kuendelea kutegemea makosa mengine huko mbeleni hasa wakati wa upigaji kura na utangazwaji wa matokeo yake.

“Tumepokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa wagombea wetu yanazothibitisha ukiukwaji na ubakwaji wa demokrasia kwa kiwango cha kutisha kiasi cha kuufanya uchaguzi huu kuwa kituko.

“Kwa ujumla, uchaguzi umepoteza sifa ya kuitwa uchaguzi, hivyo tumeazimia kujitoa," Makaidi alieleza zaidi katika taarifa yake hiyo.

Kiongozi huyo wa NLD aliwataka wanachama na wagombea wao wote nchi nzima kuwa watulivu na kutojihusisha kwa lolote kuhusiana na uchaguzi huo mpaka hapo watakapotaarifiwa vinginevyo.

CHADEMA YAKOLEZA CHUMVI

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kisisitiza kuwa hakitashiriki kama kilivyotangaza na kwamba kujitoa kwake kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa uliopangwa, hakumaanishi kutoshiriki uchaguzi mkuu mwakani.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Mafunzo wa Taifa wa chama hicho, Benson Kigaila, alisema wanakwenda kupanga mikakati kwa ajili ya ushiriki wa uchaguzi mkuu mwakani ili kupata ushindi wa kishindo.

"CCM wasitarajie kukosa upinzani katika uchaguzi mkuu. Tumejitoa kwa ajili ya kuwenda kuweka mikakati ambayo tutakuja nayo katika uchaguzi huo," alisema Kigaila.

Alisema hawatakubali kuona makosa kama hayo yanayojitokeza katika uchaguzi mkuu ujao na kuwataka wanachama wao kutohofia kujitoa kwao ili kutaka haki itendeke.

"Sisi tuko 'field' (kwenye eneo la tukio) lakini Waziri yuko ofisi ndiyo maana hajui wagombea wetu walichofanyiwa. Msimamo wetu ni ule ule kwamba hatutashiriki na hata wale waliobahatika kupata nafasi za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi hawatashiriki,” alisema.

Naye Ofisa Uchaguzi wa Kanda ya Kati wa chama hicho, Justine William, alisema wagombea wote wanapaswa kuheshimu kauli ya chama ambayo imewataka kutoshiriki katika uchaguzi huo na watakaoshiriki watakuwa wasaliti,

TAMKO ACT WAZALENDO

Ngome ya Wanawake wa chama ACT-Wazalendo, imemtaka Rais John Magufuli kukutana na viongozi wa vyama vya siasa ili kupata maridhiano na muafaka wa kisiasa kwa maslahi ya taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti Chiku Abwao, alitaja mambo 12 wanayotaka yafanyike ili kuwa na uchaguzi huru na haki.

Alisema wanaunga mkono msimamo wa chama na kwamba kushiriki uchaguzi huo ni kubaka demokrasia kwa kuwa si wa haki, huru, wazi na hauna uwanja sawa wa kisiasa kwa vyama vyote.

Abwao alisema wanashangazwa na Waziri Jaffo, kwa kauli mbili mbili na kuonyesha kuwa anatumika kuvuruga uchaguzi.

"Historia itamhukumu kwa kuchezea usalama na amani ya nchi. Kwa kauli yake tunahoji kwani mgombea binafsi ameruhusiwa?" alisema.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, inahitajika amani, uhuru, usawa wa kufanya shughuli za kisiasa nchini urejeshwe kama ilivyokuwa kwa awamu zilizopita kwa kile alichodai utawala wa vitisho hauwezi kuwa suluhisho la matatizo ya Watanzania ikiwamo ukosefu wa ajira, umasikini, ukosefu wa dawa hospitalini na miundombinu mibovu.

Alisema vitisho haviwezi kutunyamazisha, tutaendelea kuikosoa serikali ya CCM na kudai Haki zetu za Kikatiba kwa mujibu wa sheria.

CCM wanena

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema mchakato wa uchaguzi huo upo sawa na kutoa safu namna ambavyo kimewapanga watu wake kushiriki kuanzia ngazi ya chini hadi juu.

Akizungumza jana na waandishi wa habari, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole, alisema kama wapinzani waliona wameonewa walipaswa kukata rufani.

Alisema CCM itashiriki katika uchaguzi huo kupongeza msimamo uliotolewa hadi sasa na serikali.

•Imeandikwa na Salome Kitomari, Romana Malya (DAR) na Renatha Msungu (DODOMA)

Habari Kubwa