Wanafunzi 400 wakaa darasa moja chini

24Feb 2021
Shaban Njia
Kahama
Nipashe
Wanafunzi 400 wakaa darasa moja chini

WANAFUNZI 400 wa Shule ya Msingi Kabale katika Halmashauri ya Msalala, Kahama mkoani Shinyanga, wanakaa chumba kimoja cha darasa huku wengine wakiwa wamekaa chini kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.

waziri wa elimu, prof joyce ndalichako. picha mtandao

Shule hiyo ina wanafunzi 1,900 ikiwa na vyumba vya madarasa vinane, huku darasa moja likitumiwa kama ofisi ya walimu.

Aidha, wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili wanalazimika kusoma kwa awamu huku darasa la kwanza wakiingia asubuhi na darasa la pili wakiingia mchana.

Hayo yalibainishwa jana katika shule hiyo na Mwalimu wa Taaluma,  Kurwa Lufungulo, wakati wa kukabidhiwa vifaa vya ujenzi vilivyotolewa na kampuni ya Ako Group vyenye thamani ya Sh. milioni tano.  “Tatizo hili limesababishwa na ongezeko la wanafunzi.

Kila mwaka tuna vyumba vinane vya madarasa kimoja tunakitumia kama ofisi ya walimu na wanafunzi wanakaa watano katika dawati moja,”  alisema Lufungulo.

Naye mwanafunzi  Perepetua Leonard, alisema wanakabiliwa na uhaba wa madawati na kwamba kwa sasa  wanafunzi 1,900 wanakaa kwenye  madawati 216, huku darasa la kwanza, pili na awali wakikaa chini wakati wa masomo.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Dk.  Ntana Kilagwire,  Meneja Mkuu wa Ako Group, Athanas Kahindi, alisema wametoa mifuko 45 ya saruji, nondo 35,  mbao, mchanga malori 10 na mawe lori 10  na Sh. 600,000 ambazo zitatumika kulipa mafundi wakati wa ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Akipokea vifaa hivyo,  Dk. Kilagwire alikiri kuwapo kwa tatizo hilo na kusema kwa sasa wameunda kamati ya ujenzi ambayo itasimamia ujenzi wa madarasa mapya na kuwaomba wazazi na wadau wengine wa elimu kuchangia ujenzi huo.

Habari Kubwa