Wanafunzi wabuni ATM ya taulo za kike, waiita Chausiku

13Aug 2019
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Wanafunzi wabuni ATM ya taulo za kike, waiita Chausiku

Wanafunzi wa Chuo cha Mtakatifu Joseph cha Jijini Dar es salaam wameweza kubuni ATM ya taulo za kike, ambazo zitawekwa mashuleni, ofisini na hata kwenye saluni za kike.

mashine ya chausiku.

David Msemwa ambaye ni mmoja kati ya wabunifu wa ATM hiyo amesema mwanafunzi wa kike ama mtumiaji yoyote anaweza kujua mashine hiyo iliyopewa jina la Chausiku ilipo kupitia programu maalum kwenye simu ya mkononi.

"Mwanafunzi ama mtumiaji yoyote ataweza kujua Chausiku ipo wapi kwa kutumia simu yake, kuna programu maalum inayoonyesha uelekeo wa ATM zote za chausiku zilizo karibu yako," amesema Msemwa

Ameongeza kuwa jinsi ya kununua taulo hizo, kutakuwa na sarafu au kadi maalumu ambayo itajazwa fedha na kukabidhiwa mwanafunzi ambapo kadi hiyo itapitishwa kwenye mashine na kukatwa kiasi cha shilingi 2,000 hadi 2,500 kulingana na aina ya pedi iliyowekwa kwenye mashine.

Mkuu wa Kitengo cha Ubunifu kutoka Chuo hicho, Dk Lawrence Kerefu amesema kwa sasa mashine hiyo na vitu vingine vilivyobuniwa na wanafunzi wa chuo hicho, wameviwekea mkakati wa kuviboresha zaidi kabla ya kuanza kutumika.

"Wabunifu hawa tutawaletea watalaamu kutoka nje kwa ajili ya kuwafundisha zaidi ili kupata bidhaa ama mashine zilizo kwenye viwango vya kimataifa na bora zaidi,'' amesema Dk. Kerefu

Kwa sasa mashine ya Chausiku haijaanza kutumika ikitarajiwa kutumika wakati wowote kuanzia mwakani baada ya kuboresha kulingana na mazingira huku wanufaika wa kwanza wakiwa ni wanafunzi wa Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo.

Imeandikwa na Juster Prudence na Rahma Kisilwa, TUDARCO

Habari Kubwa