Wapewa elimu kunawa mikono kukabiliana na magonjwa mlipuko

16Oct 2020
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Wapewa elimu kunawa mikono kukabiliana na magonjwa mlipuko

WANAFUNZI wa Shule za Msingi na Sekondari Manispaa ya Shinyanga, wamepewa elimu ya kunawa mikono ili kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, kikiwamo kipindupindu pamoja na kuhara.

Wanafunzi wa shule ya msingi Ibinzamata manispaa ya Shinyanga, wakipewa elimu ya kunawa mikono.

Elimu hiyo imetolewa na maofisa afya wa manispaa hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Uholanzi (SNV), katika kuadhimisha siku ya unawaji mikono duniani.

Mkuu wa Idara ya Usafi na Mazingira Manispaa ya Shinyanga, Kuchibanda Snatus, akizungumza jana wakati kuhitimisha elimu hiyo ya unawaji mikono katika Shule ya Msingi Ibanzamata, amewataka wanafunzi wakawe mabalozi wazuri kwenye familia zao.

Alisema kwa utafiti ambao waliufanya mwaka 2018, asilimia 82 ya wananchi wa Shinyanga hawana vifaa vya kunawa mikono kwa sabuni, na hivyo kuwataka wanafunzi hao wakaibadilishe jamii ili kuzingatia unawaji wa mikono salama, ili kujikinga na magonjwa ya mlipuko yatokanayo na uchafu.

Mkuu wa Idara ya Usafi na Mazingira Manispaa ya Shinyanga, Kuchibanda Snatus, akitoa elimu ya kunawa mikono kwa wanafunzi.

“Manispaa ya Sinyanga tunatekeleza mradi wa usafi wa mazingira kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Uholanzi (SNV), na katika kuadhimisha siku ya unawaji mikono duniani, tukaja na mpango wa kutoa elimu ya unawaji mikono mashule, kwa kutoa elimu kwa wanafunzi ili wawe mabalozi wazuri kwenye familia zao,” alisema Snatus.

Naye Afisa kutoka SNV, Issack Msumba, aliwataka wanafunzi waizingatie elimu hiyo, ambayo itakuwa na faida kwao katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, na kubaki wakiwa salama katika maeneo ya shule ambayo yana msongamano.

Mwalimu wa afya katika Shule ya Ibinzamata, Mkami Matutu, akielezea namna wanavyokabiliana na magonjwa ya mlipuko shuleni hapo licha ya janga la corona kuisha.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Ibinzamata, Manispaa ya Shinyanga wakipewa elimu ya kunawa mikono, ili kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.
Afisa kutoka Shirika la Maendeleo la uholanzi (SNV) Issack Msumba, akitoa elimu ya kunawa mikono kwa wanafunzi ili kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Kwa upande wa Mwanafunzi aliyepata elimu hiyo, Amina Sayi, alisema wamefurahia utolewaji wa elimu hiyo, pamoja na kupewa kifaa cha kisasa ambacho watakuwa wakikitumia kunawa mikono kwa sabuni hasa pale wanapokuwa wakitoka kujisaidia.

Habari Kubwa