Wanafunzi 11 wafurahishwa na ufadhili wa masomo yao

11Apr 2017
Godfrey Mushi
Kilimanjaro
Nipashe
Wanafunzi 11 wafurahishwa na ufadhili wa masomo yao

WANAFUNZI 11 wanaofadhiliwa na taasisi ya BMFSF inayomilikiwa na Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Martin Shao, kwa ajili ya kupata elimu ya msingi, sekondari na ya juu wameeleza kufurahishwa kwao na mpango huo.

askofu Dk. Martin Shao.

Ambao unaolenga kuzinusuru familia maskini.

Mwakilishi wa wanufaika hao, Nora Amos, anayesomea stashahada ya umeme wa majumbani katika Chuo cha Ufundi Bomang’ombe kinachomilikiwa na dayosisi hiyo, jana alisema utaratibu huo ukitumiwa vizuri na mashirika mengine, watu binafsi na asasi za kiraia unaweza kupunguza mahitaji ya wanaotaka ufadhili wa elimu.

“Nimelazimika kuwaeleza Watanzania wenzangu haya kwa sababu mimi nimesaidiwa kufika hapa na watu wenye mapenzi na nia njema ya kuzibeba familia masikini nazo ziweze kupata elimu kama zilivyo familia nyingine.

Askofu mstaafu tunamshukuru kwa ufadhili na tunaomba mashirika mengine yaige taasisi hii,” alisema Nora.

Taasisi ya Askofu Dk. Shao imejitwisha jukumu zito la ufadhili wa familia masikini zenye yatima na wasiojiweza katika wilaya za Moshi, Hai na Siha waweze kujiunga na shule za sekondari na vyuo ya elimu ya juu.

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu mkakati wa kutanua wigo wa huduma hiyo, Mkurugenzi na mwasisi wa taasisi hiyo Dk. Shao alisema ufadhili huo ni wa mwaka 2017, lakini unaweza kuongezeka ili kuwasaidia wengine kumudu gharama za masomo na kujikimu.

Kwa mujibu wa Dk. Shao, kabla ya udhamini huo kutolewa kwa familia hizo, bodi ya taasisi hiyo ilipokea maombi kutoka kwa wahitaji mbalimbali na kuyahakiki na kisha kufikia uamuzi wa kutoa msaada kuendana na malengo ya taasisi.

Mbali na ufadhili huo, pia wanafunzi hao wamewezeshwa kulipia gharama za huduma za afya na matibabu kwa kushirikiana na hospitali au vituo vinavyotoa huduma za afya.

Habari Kubwa