Wanafunzi 30,675 elimu ya juu wapata mikopo

17Oct 2019
Dotto Lameck
Dar es Salaam
Nipashe
Wanafunzi 30,675 elimu ya juu wapata mikopo

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza orodha ya awamu ya kwanza yenye wanafunzi 30,675 wa mwaka wa kwanza kwa mwaka wa masomo 2019/2020 waliofanikiwa kupata mikopo yenye thamani ya TZS 113.5 bilioni.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru.

Akizungumza na waandishi habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, amesema katika orodha hiyo, wanaume ni 19,632 sawa na asilimia 64 na wanawake ni 11,043  sawa na asilimia 36.

Amesema kuwa katika orodha ya awamu ya kwanza yenye wanafunzi 30,675, wapo wanafunzi 6,142 ambao ni yatima au wamepoteza mzazi mmoja, wenye ulemavu 280 na wengine 277 wanaotoka katika kaya zinazofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Badru amefafanua kuwa waombaji wanapaswa kufungua akaunti ya SIPA (Student’s Individual Permanent Account)  ili kupata taarifa za mikopo.

“Orodha kamili ya wanafunzi hao inapatikana katika tovuti ya Bodi (www.heslb.go.tz) na pia itatumwa vyuoni ili kuwawezesha wanafunzi kufanya usajili na kuendelea na masomo, na pia Orodha nyingine itatolewa kabla ya tarehe 25 Octoba mwaka huu” Amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uchambuzi na Upangaji Mikopo wa HESLB, Dkt. Veronica Nyahende ametoa wito kwa wanafunzi ambao taarifa zao hazijakamilika kukamilisha ili wenye sifa wapangiwe mikopo. 

“Takribani wanafunzi 1,000 maombi yao hayajakamilika, watumie muda huu hadi tarehe 19 kukamilisha ili wenye sifa nao tuwapangie mkopo.

Habari Kubwa