Wanafunzi 4,000 wawekwa kambini kijiandaa mitihani

19Jul 2019
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Wanafunzi 4,000 wawekwa kambini kijiandaa mitihani

JUMLA ya wanafunzi 4,133 wa darasa la saba toka shule za msingi 106 za Halmshauri ya Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi, wamewekwa katika kambi za taaluma ili kujiandaa na mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Rukia Muwango.

Wanafunzi hao waliwekwa kambini tangu Julai 9 na watakuwa huko hadi Septemba 10 mwaka huu, wakiwa tayari wamepata muda wa kutosha wa kufundishwa na hata kujifunza.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya hiyo, Rukia Muwango, hiyo ni mara ya kwanza kwa wilaya yake kuweka kambi ya taaluma na anaamini itasaidia wanafunzi kufanya vizuri kwenye mtihani huo.

"Zipo kambi 34, zimewekwa maeneo mbalimbali ya kata za wilaya ya Nachingwea...mimi nimetoa Sh. milioni moja ikiwa ni mchango wangu kwa ajili ya kufanikisha kambi hizo," alisema Muwango.

Alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu na kuwataka walimu kufundisha kwa kufuata ratiba waliojiwekea na kuwa walezi wazuri wa watoto ili kambi hizo ziwe na mafanikio.

"Lengo letu ni kutaka watoto wasipoteze muda kwa mambo yasiyowahusu, ndio maana tumewaweka katika kambi ili waweze kujiandaa vya kutosha kwa ajili ya mtihani wa mwisho," alisema.

Mkuu huyo wa wilaya pia anawaomba wadau wa elimu kujitokeza kwa wingi kuunga mkono kambi hizo kwa vile bado zina upungufu wa chakula na mahitaji mengine muhimu kwa ajili ya wanafunzi.

Naye Ofisa Elimu Msingi, Makwasa Bulenga, alisema wilaya ina matarajio makubwa ya kambi hiyo, kwamba zaidi ya wanafunzi 3,720 watafaulu ikiwa ni sawa na asilimia 90.

"Kimkoa, wilaya yetu imekuwa ikishika nafasi ya tatu kati ya wilaya sita za mkoa wa Lindi, lakini safari hii tunaweza kufanya vizuri zaidi kwani ni mara yetu ya kwanza kuweka kambi," alisema Bulenga.

Alifafanua kuwa katika mtihani wa mwaka jana, wanafunzi 3,611 walifanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi na kwamba wavulana 1,260 na wasichana 1,409 walifaulu mtihani huo sawa na asilimia 73.91.

"Kwa Nachingwea ni mara kwanza kuweka kambi, kwani tulikwama kuanza miaka ya nyuma kutokana na changamoto mbalimbali ikiwamo baadhi ya watu kutoona umuhimu wa kambi hizo na hivyo kujiweka pembeni," alisema.

Ofisa elimu huyo alisema, wazazi wameshaelimishwa, mwitikio wao katika uchangiaji wa kambi za taaluma unaridhisha kwa vile hadi sasa zaidi ya asilimia 80 wamekamilisha michango yao.

“Yaani mtazamo wao kuhusu kambi hizi ni chanya, kwani wengi wao wamechangia vyakula, kuanzia mahindi, maharage au mbaazi na sukari kwa ajili ya watoto wao waliopo kambini muda wa miezi miwili," alisema.

Bulenga, alisema hakuna mwanafunzi aliyeachwa nyumbani eti kwa sababu mzazi au mlezi hajachangia chochote, bali wote wamewekwa kambini huku juhudi za kufuatilia michango hiyo zikiendelea.