Wanafunzi 58 wafutiwa matokeo kwa udanganyifu

16Jan 2017
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Wanafunzi 58 wafutiwa matokeo kwa udanganyifu

BARAZA la Mitihani (Necta), limefuta matokeo ya watahiniwa 58 wa kidato cha pili na darasa la nne, waliobainika kufanya udanganyifu katika mitihani ya upimaji wa kitaifa iliyofanyika Novemba mwaka jana.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde, alisema licha ya udanganyifu huo watahiniwa hao wataruhusiwa kurudia mitihani hiyo.

Katika mtihani wa taifa wa kumaliza darasa la saba wa Oktoba mwaka jana, watahiniwa 238 walifutiwa matokeo kutokana na kuhusika na udanganyifu.

Necta ilizitaja shule zilizohusika na udanganyifu huo na wilaya zake kwenye mabano kuwa ni Tumaini (Sengerema), Little Flower (Serengeti), St. Getrude (Madaba Ruvuma), Mihamakumi, Kondi, Kasandalala (Sikonge-Tabora) na Qash (Babati).

Katika mtihani, miongoni mwa udanganyifu uliogunduliwa ni walimu kuwafanyia mtihani wanafunzi wakiwa chooni, wanafunzi kuandika majibu kwenye nguo na wengine kwenda kuchukua majibu kwenye nyumba za walimu, mabweni na chooni.

Aidha, baadhi ya wasimamizi wa mitihani hiyo walidaiwa kuhusika na kwa pamoja walikabidhiwa kwa Wizara inayoshughulika na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa ajili ya kuchukuliwa hatua mbalimbali za kisheria.

Katika mtihani wa kujipima wa kidato cha pili, alisema Dk. Msonde, watahiniwa 31 walibainika kufanya udanganyifu.

Akizungumza na Nipashe, Dk. Msonde alifafanua kuwa wanafunzi 16 walikamatwa na vikaratasi vya majibu, karatasi za majibu 11 zilikutwa na miandiko tofauti ikionyesha waliandikiana, wawili walibadilishana karatasi za mitihani na wawili walifanyiana mitihani.

Kwa mtihani wa darasa la nne, watahiniwa 27 wamefutiwa matokeo kwa udanganyifu, alisema.

Alifafanua kuwa wanafunzi hao walibainika kufanyiwa mtihani na wanafunzi wa darasa la tano na la sita na kwamba pamoja na kurudia, hatua za kisheria zitachukuliwa kwa waliohusika kuruhusu kuwepo kwa udanganyifu huo.

“Baraza limeziagiza mamlaka zinazohusika kuwachukulia hatua wale wote waliohusika kwa namna moja au nyingine kusababisha kutokea kwa udanganyifu kwenye upimaji kidato cha pili na darasa la nne kwa kujibu wa kanuni za utumishi na sheria za nchi, alibainisha Dk. Msonde.

Habari Kubwa