Wanafunzi 65 wapewa ujauzito kwa miezi sita

25Jun 2019
Said Hamdani
LINDI
Nipashe
Wanafunzi 65 wapewa ujauzito kwa miezi sita

WANAFUNZI 65 wa shule za msingi na sekondari mkoani Lindi, wamekatishwa masomo baada ya kupewa ujauzito kwa kipindi kisichopungua miezi sita sasa.

Wilaya ya Kilwa inatajwa kuongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya waathirika.

Mkuu wa Mkoa huo, Godfrey Zambi, ndiye aliyefichua hayo kwenye kikao maalumu cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Lindi, kujadili Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Zambi alitaja idadi hiyo kwa lengo la kuunga mkono kauli ya Katibu Tawala wa mkoa huo, Rehema Seifu Madenge, alipoeleza tatizo la watoto wa kike kupewa mimba za utotoni, na kuwa linaendelea kushamiri, hivyo kurudisha nyuma ndoto zao za baadaye.

Zambi alisema wanafunzi hao 65 wakiwamo wawili wenye umri wa miaka 13, wanaosoma darasa la tatu, walipewa ujauzito kuanzia Januari Mosi hadi Juni 20, mwaka huu.

Zambi aliitaja Wilaya ya Kilwa inayoongoza kwa kuwa na mimba 33, Liwale (13), Lindi (9), Nachingwea (6) na Ruangwa (4).

Alisema tatizo hilo linaweza kupungua ikiwa viongozi, watendaji, wazazi na walezi watakuwa tayari kushirikiana na serikali kuwabaini na kutowaficha wanaume wanaohusika na vitendo vya kuwashawishi watoto.

Zambi aliwaeleza madiwani kwamba tatizo la mimba kwa watoto wadogo lisipodhibitiwa, upo uwezekano mkubwa ndoto za watoto wa kike zikaishia njiani, hali itakayosababisha kukosa wataalamu wanaotokana na jinsia hiyo kutoka mkoani Lindi.

“Tutawapataje wataalamu wa kike, wakiwamo manesi na fani mbalimbali ikiwa mimba zinaendelea kushamiri ndani ya mkoa wetu?” Alihoji Zambi.

Habari Kubwa