Wanafunzi 76 shule ya wasichana Mkuza wanasurika kifo

16May 2022
Julieth Mkireri
PWANI
Nipashe
Wanafunzi 76 shule ya wasichana Mkuza wanasurika kifo

MOTO umezuka katika bweni la Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkuza iliyopo Kibaha mkoani Pwani na kuteketeza vitu vya wanafunzi vikiwemo nguo na daftari.

Tukio hilo lilitokea usiku wa Mei 15 majira ya saa moja wakati wanafunzi 75 kati ya 76 wakiwa darani kujisomea.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amefika eneo la tukio muda mfupi baada ya tukio ambapo amesema mwanafunzi mmoja ndiye aliyekuwa katika bweni hilo wakati moto unatokea na alifanikiwa kuokolewa.

Kunenge amesema bweni hilo ambalo lina wanafunzi 76, kati yao 13 ndio waliopata mshtuko na kupelekwa katika hospitali ya Tumbi kwa ajili ya matibabu.

Amewataka wazazi kuondoa hofu kwani hakuna mwanafunzi aliyejeruhiwa katika tukio hilo na kwamba wote wameshapata mahala pakufadhiwa wataendelea na masomo kama kawaida.

Kamanda  wa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji Mkoa Pwani Jenifa Shirima akiwa katika tukio hilo amepongeza ushirikiano uliotolewa na wananchi kwa kutoa taarifa za tukio hilo mapema.

Makamu mwenyekiti  wa bodi ya shule hiyo Elisante Ngure ameelezea kuwa wakati tukio hilo la moto likitokea wafaunzi walikuwa wapo kwenye ibada hivyo hakuna mtoto yeyote aliyepata madhala.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dk Alex Malasusa ameushukuru uongozi wa Mkoa wa Pwani pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kwa ushirikiano wao katika tukio hilo.

Habari Kubwa