Wanafunzi afya waonywa udanganyifu wa mitihani

15Jan 2022
Neema Hussein
Katavi
Nipashe
Wanafunzi afya waonywa udanganyifu wa mitihani

WANAFUNZI wa Chuo cha Afya Mpanda mkoani Katavi, wametakiwa kuwa waaminifu na kuepuka udanganyifu katika masomo hasa kipindi cha mitihani kwa kuwa fani wanazosomea ni nyeti kwa maisha ya binadamu.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, alisema hayo jana wakati akizungumza na wanafunzi na watumishi wa chuo hicho baada ya kukabidhiwa madarasa yaliyojengwa kwa ufadhili wa Christian Social Services Commission (CSSC).

Mrindoko aliipongeza Wizara ya Afya kwa kuhakikisha chuo hicho kinafanya kazi kwa mara nyingine ikiwa ni baada ya kufungwa kwa miaka mingi.

"Nichukue nafasi hii kuwaomba Wizara ya Afya kuendelea kukisimamia chuo hiki tukishirikiana na sisi watumishi wa mkoa kuhakikisha watumishi wanapatikana kwa idadi inayotakiwa ili masomo yatolewe vizuri," alisema Mrindoko.

Mkuu wa Chuo hicho, Lightness Michael, alisema chuo kinakabiliwa na upungufu wa walimu, vitabu vya kufundishia, madarasa na ofisi za walimu. Alisema kwa sasa chuo kina walimu 10 na wanafunzi 119  huku walimu hao wakiwa saba wa kudumu na watatu wa muda.

"Chuo hiki kilianza mwaka 1974 kikasimama mwaka 1996. Baada ya hapo kwa juhudi ya Wizara ya Afya na ofisi yako, kikaanza tena mwaka mwaka 2020 kwa kuanza na wanafunzi 50," alisema.

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mpanda, Eusebius Nzigirwa, aliyeiwakilisha CSSC, alisema wanatoa huduma za kijamii ambazo ni wito uliotoka kwa Mungu wa kumhudumia mwanadamu kiroho, kimwili na kiakili.

"Sisi tumekuja kuwakilisha wenzetu kukabidhi darasa jipya na maabara iliyokarabatiwa kwa marafiki na wadau wa CSSC. Sisi tunafanya huduma zetu na tunahitaji msaada wa kiserikali na muda wote tumekuwa tukifanya nao kazi na ni wadau wakubwa wa serikali," alisema.

Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Magharibi, Sospeter Magesse, alisema wamekabidhi meza 100 na viti 100 vyenye thamani ya Sh. milioni 10 ambavyo vitatumiwa na wanafunzi kwenye darasa lililojengwa.

"Benki yetu imeendelea kuyafanya haya na si mara ya kwanza. Benki yetu imekuwa ikitenga asilimia moja kila mwaka kuipeleka kwenye sekta za afya na elimu kwa sababu tunajua tukiwa na taifa lenye afya, tutafanya maendeleo na tukiwa na watu wenye elimu, tutafanya maendeleo. Kwa hiyo afya na elimu ni sekta za kipaumbele," alisema Magesse.

Habari Kubwa