Wanafunzi Ilala kupatiwa mafunzo usalama barabarani

29Feb 2016
Romana Mallya
Nipashe
Wanafunzi Ilala kupatiwa mafunzo usalama barabarani

WANAFUNZI kutoka shule za msingi 18 za wilaya ya Ilala, wanatarajia kuanza mafunzo ya usalama barabarani kwa miezi mitatu.

Wanafunzi wakipewa mafunzo ya usalama barabarani

Mafunzo hayo yanafanyika baada ya wilaya hiyo kukabidhiwa vifaa vya kuwawezesha kuvuka barabara ili kukabiliana na tatizo la ajali.

Wakati elimu hiyo ikitolewa kwao, yako matukio kadhaa ambayo yamewahi kutokea katika barabara tofauti jijini Dar es Salaam likiwamo la Bunju B la mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi ya Bunju A, Thabitha Omari (11), kufariki dunia baada ya kugongwa na gari kisha wananchi kuchoma kituo cha polisi eneo hilo.

Ofisa Elimu ya Ufundi wa Manispaa ya Ilala, Helen Peter, alipokea vifaa hivyo jana kwa niaba ya serikali kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa CFAO Motors Group, Eric Potin.

Akizungumza baada ya kukabidhi vifaa hivyo, Potin alisema wanaamini vitasaidia kupunguza ajali zinazotokea wakati wanafunzi wanapovuka barabara.

Alisema msaada huo ni katika kuunga mkono mradi wa Ujerumani wa fursa za kimataifa (OIG) katika kusaidia programu za elimu.

Alisema kampuni yake imeamua kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule hizo pamoja na kukabidhi vifaa hivyo kupunguza ajali kwa wanafunzi wanaotumia barabara.

“Wanafunzi wanatakiwa kupewa kwanza elimu ya jinsi ya kuvuka barabara. Hii itawasaidia watakapoanza kutumia vifaa hivi wavuke kwa usalama zaidi kwa kufuata sheria za usalama barabarani,” alisema.

Pia alisema wametoa vifaa vya michezo kwa watoto hao ambavyo vitawezesha kushiriki programu mbalimbali za michezo zitakapoandaliwa katika mashule yao.

Aidha, alisema katika kuunga mkono elimu, jana magari 18 ya Volkswagen yameanza mbio za magari zijulikanazo kama ‘Go4 school’. Safari ya mbio hizo imeanzia Dar es Salaam kwenda Kigali, Rwanda, ambako yatauzwa na mengine ili kufanikisha hilo.

Alisema magari hayo yatapita Kenya na baadaye Uganda na kilele cha mshindano ni Machi 12, mwaka huu, nchini Rwanda.

Habari Kubwa