Wanafunzi nchini wananafasi ya kutoa ushindani EAC

11Dec 2019
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
Wanafunzi nchini wananafasi ya kutoa ushindani EAC

NAIBU Waziri wa Elimu, William Ole Nasha amesema pamoja na changamoto nyingi katika elimu kuwepo nchini, bado wanafunzi wanauwezo wa kutoa ushindani katika sekta ya elimu kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na zile za jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika.

Denis Mmuni kutoka St Macmillan sekondari Dar es salaam, akipokea cheti cha ushindi wa Insha ya jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka kwa Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha

Ole Nasha amesema hayo wakati wa hafla ya kuwatunuku vyeti washindi wa kitaifa wa shindano la uandishi wa Insha za Jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika (SADC).

Naibu Waziri amesema pamekuwepo na maneno ambayo yakiendelea nchini kuwa elimu ya Tanzania haina ubora kumbe hali ni tofauti kiuhalisia kwani vijana wamekuwa wakitoa ushindani kutoka katika jumuiya hizo.

"Nawapongeza sana washindi wa shindano hili kwa sababu wamewadhihirishia watanzania kuwa elimu yetu ni bora, "amesema Ole Nasha.

Amesema huwezi kuniambia leo hii elimu yetu haina ubora wakati hawa vijana wameweza kutoa ushindani katika mashindano ya uandishi wa Insha EAC na (SADC).

Kutokana na hilo amewaagiza wakuu wa shule kuendelea kuwashawishi wanafunzi kuchangamkia fursa za mashindano kwani yanawasaidia kuongezea uwezo wa wao katika kukuza ujuzi wa lugha na maarifa kwa ujumla.

Amesema mashindano hayo yatawapa uwelewa mbalimbali wa mada za masomo mengine ambayo yatawajenga wanafunzi siku za usoni kunufaika na mtangamano wa Jumuiya hizo katika kujipima kujilinganisha na nchi nyingine.

Mbali na hilo aliwataka wanafunzi walioshinda katika mashindano hayo kuwa kichocheo kwa wengine ikiwemo kutoa hamasa ili na wengine washiriki katika mashindano ya uandishi wa Insha.

"Mashindno haya hutoa msukumo kwa wanafunzi kuendelea kushiriki hadi wanapofika vyuo vikuu, "amesema Ole Nasha.

Hivyo amesema mashindano hayo yawe sehemu ya mkakati mkubwa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Sekretariet ya Jumuiya ya maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC kwa kuandaa mashindano ya uandishi wa Insha.

Pia ameitaka Wizara ya Elimu hapa nchini na ile ya Zanzibar pamoja na Baraza la mitihani washiriki katika kutangaza, kusahisha na kuratibu mashindano hayo.

Naye Mratibu wa Mashindano hayo Sylivia Chinguwile, amesema mchakato wa kupatikana washindi huanza baada ya kikao cha wakuu wa nchi wanachama kutoa azimio.

Aidha, amesema baada ya hapo kila nchi mwanachama huwajibika kutangaza na kubainisha vigezo vya ushiriki kama ilivyoelekezwa na sekretarieti.

"insha za wanafunzi huwasilishwa wizarani baada ya kuteuliwa insha bora katika ngazi ya shule na kusahihishwa na jopo la wataalmu, "amesema Chinguwile.

Amesema jumla ya wanafunzi 13 kutoka shule mbalimbali wamefanikiwa kupata ushindi huo.

Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akiwa pamoja na washindi wa tuzo za uandishi wa Insha wa mashindano ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC)

Habari Kubwa