Wanafunzi Same wapata ujauzito kwa kubakwa

29Feb 2016
Woinde Shizza
Nipashe
Wanafunzi Same wapata ujauzito kwa kubakwa
  • “Wanafunzi wanao soma katika shule hii wanatoka vijiji vya mbali sana na wengine hutoka zaidi ya kilometa 15 hivyo inawabidi kuamka saa 11:00 alfajiri na kupitia eneo la msituni,

WASTANI wa wanafunzi wa kike nane hadi 10 katika Shule ya Sekondari Vumari, wilayani Same, mkoa wa Kilimanjaro, kila mwaka hupata mimba zinazotokana na kubakwa ama kurubuniwa na wakware kutokana na kutembea umbali mrefu zaidi ya kilometa 15 kufika shuleni hapo.

MKUU WA MKOA KILIMANJARO AMOS MAKALLA

Hayo yalisemwa na mwalimu mkuu wa shule hiyo, Philip Mzava, wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea mradi wa bweni la wasichana lilojengwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) katika kuimarisha ujirani mwema na wananchi wanaozunguka Hifadhi ya Mkomazi, wilayani humo, mwishoni mwa wiki.

Alisema ujenzi wa bweni hilo utakuwa mkombozi kwa wanafunzi wa kike ambao wamekuwa wakirubuniwa kwa vishawishi mbalimbali na baadhi yao kubakwa wakati wa kurudi nyumbani au wanapo kwenda shuleni.

“Wanafunzi wanao soma katika shule hii wanatoka vijiji vya mbali sana na wengine hutoka zaidi ya kilometa 15 hivyo inawabidi kuamka saa 11:00 alfajiri na kupitia eneo la msituni, hii ni hatari sana kwa watoto wa kike ambao wengi wao hukumbana na vishawishi na wengine kubakwa na kupata ujauzito,” alisema.

Mzava alisema ipo haja kwa wadau mbalimbali kuchangia ujenzi wa mabweni mengine ili wanafunzi wa kike waweze kulala shuleni hapo.

Alisema bweni lililojengwa na Tanapa lina uwezo wa kuchukua wanafunzi 48, wakati shule hiyo ina wanafunzi zaidi ya 200.

Mhifadhi Mkuu wa Ujirani Mwema katika Hifadhi ya Mkomazi, Deogratius Ndewario, alisema ujenzi wa bweni hilo ulioanza 2012 umegarimu Sh. milioni 80 na umekamilika kwa asilimia 95 na sehemu ndogo iliobaki ya kuweka vitanda na ukuta itakamilika hivi karibuni.

Alisema mamlaka iyo imekuwa na desturi ya kuchangia miradi ya wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo, lengo likiwa ni kuimarisha ujirani mwema kwa kuwashirikisha wananchi kulinda na kuifadhi hifadhi za taifa .

Habari Kubwa