Wanafunzi shule 1,000 sekondari, hawalijui somo la Fizikia

10Jun 2021
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Wanafunzi shule 1,000 sekondari, hawalijui somo la Fizikia

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu, amesema katika uchambuzi uliofanywa na ofisi yake ndani ya miezi mitatu, umebaini takriban wanafunzi wa shule 1,000 za sekondari, hawajawahi kukutana na mwalimu wa somo la Fizikia uso kwa uso.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu.

Aidha, amesema kuna takriban shule takribani 400 watoto wa sekondari hawajawahi kumuona mwalimu wa hisabati akiingia darasani.

Ummy ameyasema hayo leo bungeni alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti maalum (CCM), Hawa Mchafu.

Katika swali lake, Mbunge huyo alihoji serikali lini itazipatia Halmashauri za Mkoa wa Pwani walimu wa sayansi ili kukidhi mahitaji yaliyopo.

Akijibu swali hilo, Waziri Ummy amekiri kuwepo kwa uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi na uchambuzi ulifanywa ndani ya miezi mitatu umebaini hali hiyo.

“Kwa hiyo Spika tatizo hili tumeliona na tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kutupa kibali cha kuajiri walimu katika mwaka huu wa fedha 2020/21, tunakamilisha maombi ya walimu ambao wameomba nafasi hizi za ajira tulizozitoa na kipaumbele ni kutatua changamoto hii ya walimu wa sayansi hususan walimu wa hesabu,”alisema.

Habari Kubwa