Wanafunzi shule binafsi waendelea na masomo

26Mar 2020
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Wanafunzi shule binafsi waendelea na masomo

WAKATI shule zote nchini zimefungwa kwa siku 30 kuanzia Machi 17 mwaka huu kutokana na tishio la virusi vya corona, baadhi ya shule binafsi zimeendelea kufundisha wanafunzi wakiwa nyumbani.

Shule hizo zinaendelea na utoaji elimu kwa mtandao kwa kuwatumia wazazi kazi za kufanywa na wanafunzi na baadaye kupewa mrejesho na hata kupatiwa kazi iliyofanywa na mwanafunzi husika ili kupitiwa na walimu.

Wazazi waliozungumza na Nipashe jana jijini Dar es Salaam kuhusu utaratibu huo, walipongeza uamuzi huo wa baadhi ya shule nchini kwa kuwa unasaidia wanafunzi kuzingatia masomo wakati wakiwa nyumbani.

Baadhi ya wazazi hao pia walisema kuna kazi ambazo huwa wanazifuata shuleni za kila wiki na wapo wanaowasiliana na walimu wa madarasa husika na kutumiwa kazi hizo kwa njia ya mtandao zikiwa na majibu yake, hivyo mzazi kupewa jukumu la kusahihisha.

“Napongeza utaratibu huu, nilipigiwa simu niende nikachukue kazi za mwanafunzi kesho (leo), nimefurahi sana kwa sababu mtoto kukaa nyumbani siku 30 bila kufanya kazi yoyote kutamfanya abobee kwenye michezo na kusahau masomo ya darasani,” alisema mmoja wa wazazi hao.

Alisema ni ubunifu mzuri kwa sababu mzazi atatoa kazi za watoto na kuzisahihisha, hivyo kutawafanya wanafunzi kuendelea kujifunza.

Mzazi wa watoto wawili, Jenifer John ambaye ni mkazi wa Sinza jijini, alisema shule kutoa kazi kwa wanafunzi waliolazimika kukaa nyumbani kwa siku 30 kunawasaidia watoto kujielekeza kwenye masomo badala ya kuzurura na kucheza mitaani.

Alitoa wito kwa wazazi kuhakikisha wanasimamia watoto wao ili wafanye kazi walizopewa na walimu ili kuwasaidia katika kipindi cha mwezi mmoja walichofunga.

“Siku ya Jumatatu nilipokea ujumbe ukinitaka niende shuleni kwa ajili kuchukua kazi za watoto ambazo wanatakiwa kuzifanya ndani ya wiki moja na kutakiwa kuzirejesha ili zisahihishwe na kupewa nyingine,” alisema.

Nipashe pia imebaini baadhi ya shule za serikali, hasa za vipaji maalum, nazo zinatoa kazi kwa wanafunzi. Shule hizo zimewapa wanafunzi vitabu na kuwataka kujisomea wakiwa nyumbani.

Mzazi wa mwanafunzi katika moja ya shule hizo za serikali jijini Dar es Salaam, alisema wanafunzi walipewa vitabu na kutakiwa kuvisoma katika kipindi chote cha mwezi mmoja wa kukaa nyumbani.

“Kama wazazi tumehimizwa na walimu kuwasimamia wanafunzi kusoma vitabu walivyonavyo na kuwasaidia masomo ambayo yanawashinda ili kuwafanya waendelee kusoma wakati wote wa likizo, ni jambo jema,” alisifu.

Machi 17 mwaka huu, serikali kupitia kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ilitangaza kuzifunga shule zote kuanzia awali hadi kidato cha sita, na siku moja baadaye ikafunga vyuo vikuu na vya kati ikiwa ni hatua mojawapo za kukabiliana na maambukizo ya virusi vya corona.

WIZARA KUTOA TAARIFA LEO

Jana, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, aliahidi kutoa taarifa leo kuhusu hali ya ugonjwa huo nchini.

Habari Kubwa